YANGA inaendelea kupiga hesabu zake na kazi kubwa sasa ni kutafuta wachezaji 23 wazawa msimu ujao, kwa sasa kuna mazungumzo yanafanyika na kiungo mmoja fundi wa kikosi cha Taifa Stars, wakitaka kumrudisha kuja kucheza nchini.

Mabosi wa juu wa Yanga wamekuwa kwenye mazungumzo na kiungo Alphonce Mabula Msanga ambaye kwa sasa ni mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachonolewa na kocha wa zamani wa mabingwa hao, Miguel Gamondi.

Yanga inataka kumrudisha nchini Mabula baada ya kuwa anacheza nje kwa muda mrefu, ikivutiwa na uwezo wake akitumika kama kiungo mkabaji.

MABULA Pict

Mabosi wa Yanga wanafanya siri kubwa lakini Mwanaspoti linafahamu Mabula ameanza kushawishika kukubali mkataba wa mabingwa hao kurejea nchini baada ya sasa kuwa mchezaji huru kutokana na kumaliza mkataba ndani ya Shamakhi ya Azerbaijan.

Hivi sasa Mabula yupo nchini kwa mapumziko ya mwisho wa msimu, nafasi ambayo Yanga imeitumia kujifungia naye na kumpa ofa nzuri kiungo huyo ili kuongeza nguvu kwenye timu yao kwa msimu ujao.

MABULA Pict

Rafiki mmoja wa karibu wa kiungo huyo, ameliambia Mwanaspoti kwamba wakati wowote kutoka sasa hatashangaa kuona Mabula anasalia nchini akiweka wazi kwamba kiungo huyo amevutiwa na mafanikio ya Yanga lakini pia ushiriki wake kwenye mashindano ya kimataifa.

“Nikweli kaka, Mabula awali alitaka kwenda mapumzikoni nje ya nchi lakini Yanga walimzuia kuondoka kwa kuwa wana mazungumzo naye, yalianza muda sana, nadhani wanaweza kumalizana wakati wowote,” amesema rafiki huyo ambaye ni mchezaji wa Stars.

MABULA Pict

“Sitashangaa kuona Mabula anacheza Yanga kwa msimu ujao, unajua nafasi kubwa inatokana na mkataba wake na klabu yake ya mwisho umemalizika, kwa sasa ni mchezaji huru na Yanga wamempa ofa kubwa.”

Yanga itarudi tena kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao, baada ya kushindwa kufuzu kwenda robo fainali kwenye mechi ya mwisho msimu uliopita, ikiishia hatua ya makundi, ikimaliza nafasi ya tatu kwenye kundi B, ikiziacha Al Ahly na AS FAR Rabat zikisonga mbele.

MABULA Pict

AS FAR Rabat baada ya kufuzu hapo na kuinyima nafasi Yanga, ikaenda kucheza mpaka fainali ikilikosa taji hilo mbele ya mabingwa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ambapo Waarabu hao kwasasa wameshamchukua kocha wa zamani wa Yanga, Pedro Goncalves.

Mabula ambaye mwaka 2022 aliondoka Alliance FC ya Mwanza na kutua Spartak ya Serbia, amekuwa na kipindi cha miaka minne akicheza soka barani Ulaya.

Timu zingine alizozitumikia mbali na Spartak ni RFK Novi Sad ya Serbia na Shamakhi kule Azerbaijan ambayo amemaliza nayo mkataba Juni 30, 2026.

MABULA Pict

Kiungo huyo aliyezaliwa Juni 14, 2003 huko Nyamagana jijini Mwanza, hivi sasa ana umri wa miaka 23 ambapo amepita timu zote za vijana za taifa za Tanzania kuanzia ile ya chini ya miaka 17 maarufu Serengeti Boys aliyoitumikia mwaka 2019, kisha chini ya miaka 20 na sasa ya wakubwa, Taifa Stars.

Yanga inataka kuimarisha eneo la kiungo mkabaji ambapo kwa msimu wa 2025-2026, Duke Abuya na Mohamed Damaro ndiyo waliokuwa wakitumika zaidi, huku Mudathir Yahya muda mwingi akicheza kiungo wa juu.

Katika eneo hilo, Aziz Andabwile na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ walikuwa wakicheza kwa nadra sana, huku ikielezwa kwamba, Sure Boy msimu ujao hatakuwa ndani ya kikosi hicho, hivyo Yanga inamuhitaji Mabula kutokana na uzoefu alionao huku akiwa bado ni damu changa anayeweza kupambana kwa muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *