Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Mojtaba Khamenei, ameeleza shukrani zake za dhati kwa mahudhurio “ya kustaajabisha, yenye kuvunja nguvu za adui na ya kihistoria” katika mazishi ya Kiongozi Shahidi, akisisitiza kuwa malipo ya kisasi dhidi ya “watenda jinai wauaji waliodhalilika” ni jambo la yakini.

Katika ujumbe uliotolewa kufuatia shughuli za mazishi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Ayatullah Mojtaba Khamenei amesifu ushiriki mkubwa wa umma nchini Iran na Iraq, akiuita kuwa ni dhihirisho la kipekee la uungaji mkono.

Aidha amebainisha kuwa: “Tunaahidi kulipiza kisasi cha damu takatifu ya Kiongozi aliyeuawa shahidi na mashahidi wote wa vita hivi viwili kutoka kwa wauaji wa jinai na waliofadhaika.”

Aliongeza: “Ninatoa shukrani za dhati kwa uwepo wa mamilioni ya watu katika miji na vijiji vya Iran na Iraq, hususan Tehran, Qom, Najaf, Karbala na Mashhad.” Alielezea mahudhurio hayo kuwa ni “ya kustaajabisha, yenye kuvunja nguvu za adui na ya kihistoria.”

Akimhutubu moja kwa moja na Kiongozi aliyeuawa shahidi, Ayatullah Mojtaba Khamenei amesema, “Kwa macho yenye machozi na nyoyo zilizovunjika, tunapoaga mwili wako, tunaahidi kulinda mfumo wako wa kifikra na kufuata kwa dhati njia nyoofu uliyochora, bila kuogopa ugumu wowote na tukitawakal kwa ahadi za Mwenyezi Mungu kama ulivyofanya wewe.”

Kiongozi huyo alitangaza kuwa kulipiza kisasi cha damu ya Kiongozi Shahidi na mashahidi wote wa vita hivi viwili vya uchokozi vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran ni “takwa la taifa letu na ni lazima litekelezwe bila shaka.”

Ayatullah Mujtaba Khamenei amesema waliohusika “wataenda makaburini mwao wakiwa na ndoto ya kufa kifo cha amani kitandani,” akiongeza kuwa ahadi hiyo “haitegemei uwepo wangu au wa viongozi wengine.”

Amesema: “Iwe tupo hapa au hatupo, jambo hili litatimia, na hivi karibuni, watu huru duniani kote kila mmoja atatekeleza sehemu ya jukumu hili la takatifu.”

Ayatullah Mojtaba  Khamenei pia ametoa heshima kwa wale waliokufa shahidi pamoja na Kiongozi Shahidi, akisema, “Mumebarikiwa  kwani sasa ni wageni wa Maula (Kiongozi) mliyemtumikia kwa ikhlasi.”

Akimhutubu  Ali ibn Musa al-Rida, Imam wa nane wa Waislamu wa Shia, alimuelekezea Kiongozi aliyeuawa shahidi kama “mtumishi mnyenyekevu” ambaye alitoa kila kitu kwa ajili ya imani yake na kwa ajili ya kumtumikia Imam.

Ujumbe huo ulielezea matumaini kwamba, katika siku zijazo, atakuwa miongoni mwa waja wema watakaofuatana na Muhammad al-Mahdi, Imam mwokozi anayesubiriwa katika imani ya  madhehebu ya Shia.

Ayatullah Mojtaba Khamenei amehitimishwa kwa kutoa mkono wa pole kwa Imam wa Zaman (Imam Mahdi) na kuomba kunyanyuliwa kwa daraja za wote waliouawa.

Alibainisha kuwa, “Tunamuomba Mwenyezi Mungu awajalie mashahidi wote daraja za juu kabisa, awape subira familia zao, na alijaalie taifa la Iran lililodhulumiwa ushindi thabiti na wa haraka, Insha’Allah.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *