Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ujumbe wake wa siku hii amesema vijana wanapaswa kupewa uhuru, fursa na msaada unaohitajika ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii.

Hali ilivyo

  • Vijana wanakabiliwa na dunia iliyoathiriwa na migogoro, ukosefu wa usawa, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya teknolojia.
  • Licha ya changamoto hizo, vijana wanaendelea kuwa viongozi, wavumbuzi na wanaharakati wanaotoa suluhisho kwa matatizo yanayoikabili dunia.
  • Umoja wa Mataifa unasema nguvu na ubunifu wa vijana, pamoja na uzoefu wa vizazi vya zamani, ni muhimu katika kujenga dunia bora.

Je anataka nini kifanyike?

  • Kuongeza uwekezaji katika elimu na ujuzi wa vijana.
  • Kupanua upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango.
  • Kuimarisha fursa za ajira zenye staha kwa vijana.
  • Kuwashirikisha vijana kikamilifu katika maamuzi yanayohusu maisha yao na maendeleo ya jamii.
  • Kuhakikisha haki, uchaguzi na fursa zinapatikana kwa watu wote bila ubaguzi.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa kwa kuwawezesha vijana leo, dunia inaweza kujenga mustakabali wenye amani, haki na ushirikishwaji kwa kila mtu.

Ujumbe wa Mkuu wa UNFPA

Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, (UNFPA) Dkt. Diene Keita jambo muhimu ni kuongeza uwekezaji kwa vijana kwa kuwapatia elimu, huduma za afya ya uzazi, ajira zenye staha na nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayowahusu.

Akiunga mkono ujumbe wa Katibu Mkuu, Dkt. Keita amesema vijana wengi bado wanatamani kuoa au kuolewa na kupata watoto, lakini wanahofia kuwa ndoto hizo huenda zisitimie kutokana na ukosefu wa ajira, gharama kubwa za makazi, kuongezeka kwa ukosefu wa usawa na migogoro inayoendelea duniani.

Matokeo ya utafiti wa demografía ya siku zijazo

Amenukuu matokeo ya utafiti wa Mwelekeo wa Siku za Usoni wa Demografia uliochapishwa wiki hii ambao unaonesha si kwamba vijana hawataki kuanzisha familia, bali wanakosa uhakika wa maisha unaowawezesha kufanya maamuzi hayo.

Dkt. Keita amesisitiza kuwa serikali zinapaswa kuweka sera zinazowawezesha vijana badala ya kuwashinikiza kufanya maamuzi fulani kuhusu uzazi au familia.

Uwekezaji unaotakiwa

Amesema uwekezaji katika makazi, huduma za afya, likizo za uzazi, huduma za malezi ya watoto na fursa za kiuchumi utawapa vijana uwezo wa kupanga maisha yao na kutimiza malengo yao.

Kwa mujibu wa UNFPA, vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani wametoa ujumbe mmoja ulio wazi: wanahitaji mazingira salama, yenye fursa na yanayoheshimu haki na uchaguzi wao ili waweze kujenga familia wanazozitamani na kuchangia maendeleo ya jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *