
Wamalawi 38,000 waondoka Afrika Kusini kufuatia maandamano ghasia dhidi ya wahamiaji
Afrika Kusini imetikiswa na maandamano na machafuko ya wiki kadhaa yanayolenga wahamiaji, ambao wanatuhumiwa kuchukua nafasi za ajira na rasilimali.
Polisi ya Afrika Kusini imeeleza kuwa raia wawili wa Msumbiji, mmoja wa Malawi na mwingine wa Ethiopia wameuawa katika ghasia zinazohusiana na machafuko hayo.
Raia kutoka nchi kadhaa za Kiafrika ikiwa ni pamoja na Ghana, Nigeria, Uganda na Zimbabwe wamekuwa wakiikimbia Afrika Kusini tangu mwishoni mwa mwezi Mei huku makundi ya raia wachache wa nchi hiyo wakishinikiza kuondoka nchini humo wahamiaji wasio na vibali halali vya kuishi.
Idara ya Usimamizi wa Majanga ya Malawi imearifu kuwa raia wake sita wameaga dunia baada ya kuugua wakiwa katika safari ndefu ya kurejea nchini.
Serikali ya Zimbabwe Jumanne wiki hii iliripoti kuwa imewasaidia kurejea nyumbani kutoka Afrika Kusini raia wake karibu 21,300 tangu mwishoni mwa mwezi Mei.