Geita. Serikali kwa kushirikiana na Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) na wadau wa maendeleo, wamezindua kampeni ya kukusanya zaidi ya Sh2.6 bilioni kwa ajili ya kuimarisha mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi, huku wakiwataka Watanzania kujitokeza kuchangia ili kuhakikisha afua za kinga, upimaji na matibabu zinaendelea kutolewa.
Fedha hizo zitakusanywa kupitia kampeni ya GGM-Aids Kili Challenge, itakayohitimishwa kwa mbio za baiskeli na upandaji wa Mlima Kilimanjaro kuanzia Julai 24 hadi 30, 2026, chini ya kaulimbiu isemayo ‘Ni jukumu letu sote.’
Akizungumza katika tamasha la Health Day lililofanyika Geita Mjini leo Jumapili, Julai 12, 2026, Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Lucy Beda amesema mchango wa wananchi na sekta binafsi unahitajika ili kuziba pengo la rasilimali katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika elimu, kinga na matibabu, lakini ushiriki wa wadau utaongeza uwezo wa kuwafikia watu wengi zaidi wanaohitaji huduma.
Katibu tawala wilaya ya Geita, Lucy Beda, akizungumza kwenye tamasha la Geita Health Day linalofanyika kwa lengo la kukusanya 2.6 bilioni kufadhili afua za afya dhidi ya UKIMWI.
“Naomba tushirikiane kuchangia. Hakuna fedha ndogo linapokuja suala la kuokoa maisha ya Watanzania na kuimarisha mwitikio dhidi ya Ukimwi,” amesema Beda.
Pia amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kufahamu hali zao mapema na kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.
Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (Nacopha), Leticia Morice amesema kupungua kwa ufadhili kutoka kwa baadhi ya washirika wa maendeleo kunafanya mchango wa sekta binafsi na wadau wa ndani kuwa muhimu zaidi katika kuhakikisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo yanaendelea.
Mganga mkuu mkoa wa Geita,Dk Omar Sukari akizungumza kwenye tamasha la Geita Health Day linalofanyika kwa lengo la kukusanya 2.6 bilioni kufadhili afua za afya dhidi ya UKIMWI.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Omar Sukari amesema mkoa huo unakadiriwa kuwa na watu 95,000 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, lakini ni takribani asilimia 80 pekee wanaofahamu hali zao.
Amesema kampeni ya mwaka jana ilikusanya Sh100 milioni zilizosaidia kugharamia afua mbalimbali, huku matarajio ya mwaka huu yakiwa kukusanya zaidi ya Sh2.6 bilioni kwa ajili ya huduma za kinga, upimaji na matibabu.
Kaimu Meneja mgodi wa GGML,Duan Campbell akizungumza kwenye tamasha la Geita Health Day, kwa lengo la kuchangisha Sh2.6 bilioni kwa ajili ya kuunga mkono mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI nchini Tanzania.
Kaimu Meneja Mkuu wa GGML, Duan Campbell amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhamasisha ushiriki wa jamii katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
Amesema lengo la kampeni hiyo si kuhamasisha shughuli za michezo pekee, bali kuunganisha Watanzania katika kuchangia jitihada za Taifa za kudhibiti maambukizi mapya ya VVU na kuboresha maisha ya wanaoishi na virusi hivyo.