IRINGA: Ndoto ya kumalizika kwa ujenzi wa nyumba ya watumishi katika Kijiji cha Magunga, Kata ya Maboga, Jimbo la Kalenga imepata nguvu mpya baada ya Mbunge wa jimbo hilo, Jackson Kiswaga, kukabidhi mifuko 100 ya saruji, hatua inayotarajiwa kuharakisha kukamilika kwa mradi huo na kuwaondolea watumishi adha ya kupanga nyumba mbali na vituo vyao vya kazi.
Msaada huo unatajwa kuwa sehemu ya mchango wa Mbunge Kiswaga katika kuunga mkono juhudi za wananchi na Serikali za kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, huku wananchi wakitarajia kuukamilisha mradi huo ifikapo Oktoba mwaka huu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kiswaga alisema msaada huo ni mwendelezo wa ushiriki wake katika mradi huo, akibainisha kuwa awali alitoa bati 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga, Michael Mgimwa, alimshukuru mbunge huyo kwa msaada huo, akisema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza kasi ya ujenzi na kufanikisha lengo la kuhamishia watumishi kwenye makazi yao mapya.
Alisema kukamilika kwa nyumba hiyo kutapunguza changamoto zinazowakabili watumishi ambao kwa sasa wanalazimika kupanga nyumba mitaani kutokana na ukosefu wa makazi ya serikali.
Katika ziara hiyo, Mbunge Kiswaga pia alikutana na wananchi na kusikiliza kero mbalimbali, huku migogoro ya ardhi ikitajwa kuwa changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa eneo hilo.
