Maswa. Wakulima wa zao la pamba katika Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu, wamepewa elimu kuhusu mfumo wa kupokea malipo ya mauzo ya pamba kupitia benki na huduma za fedha kwa njia ya simu, hatua inayolenga kuongeza uwazi, usalama wa fedha na kuharakisha malipo.

Elimu hiyo imetolewa leo Jumatatu, Julai 13, 2026 na maofisa ushirika wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2026/2027.

Akizungumza mjini Maswa, Ofisa Ushirika wa TCDC, Aron Mrema amesema matumizi ya taasisi za fedha katika malipo ya pamba yatawawezesha wakulima kupata fedha zao kwa wakati, kupunguza hatari ya kupoteza fedha na kuongeza uwazi katika biashara ya zao hilo.

Amesema mfumo huo pia utasaidia kuweka kumbukumbu sahihi za malipo na kuimarisha uaminifu katika mnyororo mzima wa biashara ya pamba.

Mrema amewataka wakulima kuhakikisha wanafungua akaunti za benki au kujisajili kwenye huduma za fedha kwa njia ya simu, pamoja na kuhakiki taarifa zao kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa malipo.

Afisa Ushirika, Aron Mrema kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) akizungumza na wakulima katika chama cha msingi cha ushirika cha Sola wilayani Maswa. Picha na Samwel Mwanga

“Serikali imeendelea kuhimiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika malipo ya mazao ya kimkakati, ikiwemo pamba, ili kuongeza uwazi, usalama wa fedha na kuwajumuisha wakulima katika huduma rasmi za kifedha,” amesema.

Baadhi ya wakulima waliohudhuria mafunzo hayo kutoka Chama cha Msingi cha Ushirika cha Sola (AMCOS) walisema elimu hiyo imewapa uelewa kuhusu mfumo mpya wa malipo na kuondoa hofu waliyokuwa nayo.

Mkulima,  Joseph Bundala amesema awali, baadhi ya wakulima walikuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu namna malipo yanavyofanyika kupitia benki, hali iliyokuwa ikiwasababishia wasiwasi hasa  yalipochelewa.

“Elimu hii imetufungua macho. Sasa tunafahamu umuhimu wa kuwa na akaunti ya benki au kutumia huduma za fedha kwa simu ili malipo yetu yafike salama na kwa wakati,” amesema.

Kwa upande wake, Njile Emanuel amesema mfumo huo utawasaidia wakulima kupanga vizuri matumizi ya mapato yao na kupunguza hatari ya kutembea na fedha taslimu baada ya kuuza pamba.

Ametoa wito kwa Serikali na viongozi wa vyama vya ushirika kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kila mmoja auelewe mfumo huo na kunufaika na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya kilimo.

Afisa Ushirika, Mbaraka Maleu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) akizungumza na wakulima katika chama cha msingi cha ushirika cha Sola wilayani Maswa. Picha na Samwel Mwanga

“Tunaiomba Serikali iendelee kutuelimisha mara kwa mara ili wakulima wote wauelewe mfumo huu na wasiache kutumia huduma za kifedha zinazorahisisha malipo,” amesema.

Naye mkulima,  Jimoga Masanja amesema matumizi ya benki na huduma za fedha kwa njia ya simu yataongeza imani ya wakulima katika mfumo wa ununuzi wa pamba kwa kuwa kila malipo yatakuwa na kumbukumbu zinazoaminika.

“Tunatarajia msimu huu malipo yatafanyika kwa haraka zaidi kuliko ilivyokuwa zamani. Hilo litatupa hamasa ya kuongeza uzalishaji wa pamba,” amesema.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika sekta ya kilimo, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa malipo, kuimarisha usalama wa fedha za wakulima na kukuza ujumuishaji wa huduma rasmi za kifedha nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *