Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi imeendelea kuzaa matunda baada ya Serikali kukabidhi mradi mkubwa wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba wenye thamani ya Shilingi milioni 400 kwa vijana wa Kata ya Lupingu, Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.

Mradi huo, uliotekelezwa kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, unatajwa kuwa hatua muhimu ya kugeuza rasilimali za Ziwa Nyasa kuwa chanzo kikubwa cha ajira, uzalishaji na maendeleo ya wananchi, huku ukitoa matumaini mapya kwa vijana wengi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji na fursa za kiuchumi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya ahadi iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni, ambapo aliahidi kuhakikisha vijana na wanawake wanapata mitaji na fursa za kujenga uchumi wao kupitia miradi yenye tija.

“Mhe. Rais alipofika Ludewa aliahidi kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi. Leo tunashuhudia ahadi hiyo ikitekelezwa kwa vitendo. Hii si fedha za matumizi, bali ni uwekezaji mkubwa wa Serikali unaolenga kuzalisha ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kuuchochea uchumi wa Wilaya ya Ludewa pamoja na Mkoa wa Njombe kwa ujumla,” amesema Nanauka.

Amesema Serikali haikuishia kutoa mtaji pekee, bali imeweka mazingira yote ya kuhakikisha mradi huo unafanikiwa kwa kugharamia ujenzi wa vizimba vya kisasa, kutoa mafunzo ya kitaalamu kupitia wataalamu wa sekta ya uvuvi pamoja na kununua chakula cha samaki kwa kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.

Nanauka amesisitiza kuwa mkopo huo umetolewa bila riba, huku marejesho yakianza baada ya vijana kuvuna na kuuza samaki kwa mara ya kwanza, hatua ambayo inalenga kuwapa nafasi ya kujijenga kiuchumi kabla ya kuanza kurejesha fedha hizo.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *