
Mgogoro unaoendelea wa Marekani na Iran umefichua kwa uwazi zaidi kuliko huko nyuma, mipasuko ya kisiasa iliyopo huko Washington. Huku utawala wa Donald Trump ukisisitiza kuendeleza operesheni za kijeshi, upinzani unaongezeka bungeni, miongoni mwa umma kwa ujumla, na hata miongoni mwa baadhi ya Warepublican.
“Watu wa Marekani sasa wanalipa gharama ya kushindwa kabisa Trump kuhusu Iran.” Kauli hii ya Chuck Schumer, Kiongozi wa Chama cha Democrats katika Seneti ya Marekani, inaonyesha mgawanyiko mkubwa uliopo ndani ya Marekani kuhusu mzozo unaoendelea wa kijeshi na Iran. Akijibu taarifa rasmi ya Donald Trump kwa Bunge kwamba Marekani iko vitani tena na Iran, Schumer amekejeli kauli hiyo kwa kusema: “Rais Trump amewaarifu rasmi wabunge kwamba nchi iko vitani tena na Iran. Kweli? Asante, Donald!” Kauli hizi zinaakisi hisia za mfadhaiko katika sehemu kubwa ya tabaka la wanasiasa wa Marekani kuhusu vita ambavyo havina mwelekeo wa wazi, mkakati maalum, wala uungwaji mkono mkubwa wa umma.
Zaidi ya miezi minne imepita tangu kuanza kwa vitendo vipya vya uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran, ambavyo, kwa mtazamo wa wachambuzi wengi na hata baadhi ya wanasiasa wa Marekani, vinakosa vipengele vitatu muhimu vya kufanikiwa: Lengo la wazi, mkakati maalum na uhalali wa kisiasa. Donald Trump alizungumzia malengo makubwa mwanzoni mwa mzozo huu, lakini sasa amelazimika kulitaarifu rasmi Bunge kuhusu kuendelea vita, hatua inayoashiria kuwa si tu kwamba malengo ya awali hayajatimizwa, bali Marekani pia imeingia katika awamu ya vita vya kuchosha na vyenye gharama kubwa. Hivyo, Schumer anasisitiza kuwa msimamo wa Trump “si mkakati, bali ni kichocheo cha maafa makubwa yasiyo na mfano wake.”
Jambo la muhimu zaidi ni upinzani unaoongezeka ndani ya Marekani yenyewe. Upinzani dhidi ya kuendelea vita hauonekani upande wa chama cha Wademocrat pekee bali ripoti zinaonyesha kuibuka makubaliano kati ya vyama vyote viwili vikuu bungeni kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro uliopo na kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa Marekani. Schumer amemtaka Trump kuheshimu matakwa ya wabunge walio wengi na kufuata njia ya diplomasia badala ya kuchochea mzozo wa kijeshi. Upinzani huu haukomei ndani ya bunge pekee bali tafiti zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya raia wa Marekani hawaridhishwi na namna mzozo huu unavyoshughulikiwa. Hata baadhi ya wapigakura wa chama cha Republican hawaungi mkono kuendelezwa kwa sera hii ya uchokozi. Ndani ya kundi la “Make America Great Again” (MAGA), watu mashuhuri kama Tucker Carlson wanaona kuwa kuingia vitani na Iran ni kinyume na ahadi za kampeni za Trump za kuepuka vita vyenye gharama kubwa nje ya nchi. Mshikamano huu wa nadra kati ya wakosoaji Wademokrat na sehemu ya kambi ya Wahafidhina unaonyesha kwamba mzozo kuhusu Iran si ushindani wa vyama tena bali umebadilika kuwa suala la kitaifa nchini Marekani.
Wapinzani wa vita wanasema utawala wa Trump, bila kufikia makubaliano ya kitaifa, umeitumbukiza Marekani katika mgogoro ambao gharama zake zinawaangukia moja kwa moja raia wa kawaida wa nchi hiyo. Kuongezeka kwa matumizi ya kijeshi, mzigo kwenye bajeti ya umma, na wasiwasi kuhusu kupanda kwa bei ya nishati, na taathira zake kwenye mfumuko wa bei, ni baadhi ya sababu za kuongezeka upinzani huo huko Marekani. Akizungumzia kupanda kwa gharama za mafuta na bidhaa muhimu, Chuck Schumer anasema: “Familia za wafanyakazi za mikono zinalipa gharama kubwa katika vituo vya mafuta na maduka ya vyakula.” Kwa maoni yake, Wamarekani kwa sasa wanalipa gharama ya kushindwa kimkakati utawala wa Trump kuhusu Iran.
Sambamba na mashinikizo ya kiuchumi, wasiwasi kuhusu usalama wa wanajeshi wa Marekani pia umeongezeka. Migogoro inayoendelea, kuhatarishwa usalama wa eneo na kushambuliwa wanajeshi wa Marekani kumeibua maswali mengi miongoni mwa umma wa Marekani kuhusu lengo halisi la vita hivi vinavyoendelea. Wakosoaji wanasema kutangazwa usitishaji vita huku shughuli za kijeshi zikiendelea sio tu kumeshindwa kubadilisha ukweli uliopo nyanjani bali pia kunaondoa imani ya umma kwa utawala. Katika ngazi ya kimataifa, uchokozi mpya wa Marekani pia umekabiliwa na ukosoaji mkubwa. Serikali nyingi na mashirika ya kimataifa yanasisitiza haja ya kupunguzwa mvutano, kuheshimiwa sheria za kimataifa na kurudi kwenye njia ya diplomasia. Uzoefu wa miongo miwili iliyopita, kuanzia Afghanistan hadi Iraq, unaonyesha kuwa uingiliaji wa kijeshi wa Marekani sio tu umeshindwa kudhamini usalama bali pia umechochea ghasia na kusababisha gharama kubwa za kiuchumi na migogoro mikubwa ya kibinadamu. Kwa hivyo, wachambuzi wengi wanaonya kwamba kuongezeka kwa mgogoro na Iran kunaweza kuhatarisha zaidi usalama wa nishati, biashara ya kimataifa na utulivu katika Asia Magharibi. Taathira jumla za matukio haya zinaonyesha kuwa utawala wa Trump si tu unakabiliwa na mashinikizo yanayoongezeka na kutengwa kidiplomasia kimataifa, bali pia na upinzani mkubwa usio na kifani ndani ya nchi, kutoka kwa umma, bunge na hata makundi ya kisiasa ndani ya kambi yake mwenyewe. Kinachoendelea Washington leo ni mzozo kuhusu mustakabali wa sera za nje za Marekani na gharama kubwa za vita ambavyo hata wakosoaji ndani ya mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo wanavieleza kuwa “janga lisilo na mfano wake” na “kushindwa kimkakati” kwa utawala wa nchi hiyo.