
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuwasimamisha kazi masheikh watatu wa mikoa kwa kukiuka misingi ya baraza hilo, baadhi yao wamefunguka kuhusu uamuzi huo.
Uamuzi wa kuwasimamisha uongozi masheikh hao, akiwemo wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Kawambwa, ulitangazwa jana Jumanne, Julai 14, 2026, na Kaimu Mufti wa Tanzania ambaye pia ni Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ali Ngeruko.
Kwa mujibu wa Sheikh Ngeruko, uamuzi huo ulifikiwa baada ya kikao cha dharura kilichoketi, ambacho kiliwasimamisha uongozi masheikh wengine, Issa Nasor wa Mkoa wa Singida na Sheikh Hassan Kiburwa wa Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Julai 15, 2026, Sheikh Kiburwa amesema amepokea uamuzi huo na anauheshimu, akisema ni utaratibu wa kawaida wa kubadilisha uongozi kutokana na mifumo ya Bakwata.
“Kama kiongozi wa dini lazima niupokee uamuzi uliotolewa. Nasubiri nipate barua rasmi ya kusimamishwa uongozi, kisha nitasema. Hawajaniambia kosa langu, sijaitwa kusikilizwa, labda nitaelezwa katika barua ya kusimamishwa,” amesema.
“Napokea kwa mikono miwili uamuzi wa Baraza la Ulamaa ambalo ni chombo cha mamlaka ya juu cha Bakwata. Wakishasema, wamesema. Nimesikia hizi taarifa kama nyie mlivyozisikia, bado sijaambiwa rasmi,” amesema Sheikh Kiburwa.
Kwa upande wake, Sheikh Nasor ameungana na Sheikh Kiburwa kupokea uamuzi wa Baraza la Ulamaa, akisema kilichotolewa na ngazi za juu lazima kipokelewe.
“Tumepokea tukitambua kwamba tunaendesha majukumu yetu kwa kuachiana kijiti. Nimepokea na namshukuru Mungu. Tunaendesha mambo yetu kupitia mipango aliyoipanga Mungu, huenda Mungu ndiye amepanga niongoze na kuishia hapa,” amesema Sheikh Nasor.
Kuhusu makosa anayodaiwa kutuhumiwa, Sheikh Nasor amesema hawezi kuzungumza sana kwa sababu baraza hilo ndilo linalojua kama amekiuka maadili au la.
“Kwa sababu wakubwa zangu ndio wamesema, wao ndio wanajua nimekiuka wapi. Siwezi kushindana nao. Tuna haki ya kupokea uteuzi na unaposimamishwa pia,” ameeleza Sheikh Nasor.
Jitihada za kumpata Sheikh Walid zimegonga mwamba baada ya simu yake kutopatikana.
Taarifa ya kusimamishwa
Kwa mujibu wa taarifa ya jana Jumanne ya Sheikh Ngeruko, uamuzi wa kuwasimamisha umechukuliwa kutokana na mienendo inayokwenda kinyume na misingi ya uongozi wa kibaraza.
“Kikao cha dharura cha Baraza la Ulamaa kimeazimia kumsimamisha Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na mienendo inayokiuka misingi ya uongozi ya kibaraza,” imeeleza taarifa hiyo.
Baada ya kusimamishwa kwa Sheikh Walid, Baraza hilo limemteua Sheikh Abbas Ramadhani Abbasi, ambaye alikuwa mjumbe wa Baraza la Masheikh Mkoa wa Dar es Salaam, kuwa Kaimu Sheikh wa mkoa huo.
Kwa upande wa Mkoa wa Singida, nafasi hiyo itakaimiwa na Sheikh Issa Simba, huku Mkoa wa Kigoma ukiongozwa kwa muda na Sheikh Uwesu Kiumbe.
Bakwata haijaeleza kwa kina aina ya mienendo iliyosababisha hatua hiyo ya kinidhamu, ikisema uamuzi huo umezingatia misingi na taratibu za uongozi wa taasisi hiyo.
Hata hivyo, jana akizungumza na Mwananchi kwa simu, Katibu Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Ulamaa, Sheikh Hassan Chizenga, alisema masheikh hao wamekwenda kinyume na maadili ya uongozi wa baraza.
“Ninachoweza kusema ni kweli hawa wamesimamishwa kwa kwenda kinyume na maadili ya uongozi wa baraza. Naomba niishie hapo. Kwa mujibu wa dini yetu, kueleza kwa undani kuhusu hili ni makosa.”
Akijibu kuhusu hatua hiyo ya kuwasimamisha itachukua muda gani, Sheikh Chizenga alisema, “Tutafanya uchunguzi wa kina. Hata huko kusimamishwa kwao ni kupisha uchunguzi, halafu baadaye kama itadhihiri vinginevyo, basi tutaangalia nini cha kufanya,” amesema.