Dar es Salaam. Kila asubuhi hufika pembezoni mwa barabara ya Kilwa eneo la Mbagala Zakhiem akiwa na mataulo na vitambaa vya kufutia vioo vya magari, hubeba bidhaa hizo kwa matarajio ya kuziuza ili kupata fedha za matumizi ya familia yake.
Kwa miaka kadhaa, eneo hilo limekuwa ndilo soko lake, likimpa wateja wanaopita kwenye magari na watembea kwa miguu. Lakini nyuma ya kila mauzo anayopata, kuna hofu kubwa inayomwandama kila siku, ya kugongwa na magari yanayopita kwa kasi.
“Wakati mwingine unauza huku macho yako yakiwa barabarani. Unasikia honi, unaona magari na bodaboda vikipita karibu sana na eneo ulilokaa. Kila siku anaondoka nyumbani hujui kama utarudi salama,” amesema.
Asha ni miongoni mwa maelfu ya wafanyabiashara wadogo wanaouza bidhaa zao kandokando ya barabara, kwenye vituo vya daladala, maeneo ya taa za kuongozea magari na maeneo yenye msongamano wa watu.
Kwao, barabara imekuwa sehemu ya kutafuta riziki, lakini pia imekuwa eneo linalowaweka kwenye hatari kubwa ya ajali, ukatili, kupoteza bidhaa na wakati mwingine kupoteza maisha.
Foleni za magari fursa
Katika miji mingi nchini Tanzania, hasa Dar es Salaam, wafanyabiashara wa bidhaa ndogo wamekuwa wakivutiwa na maeneo ya barabarani kutokana na wingi wa watu na magari.
Wauzaji wa matunda, maji, vitafunwa, ice cream, mihogo mibichi, nguo, vifaa vya simu, vifaa vya magari, viatu na bidhaa mbalimbali wamekuwa wakitumia muda ambao magari yamesimama kwenye foleni kuwafikia wateja.
Kwa baadhi yao, eneo hilo ndilo linalowezesha kupata riziki ya kila siku, hivyo hawaoni mbadala wa kuhatarisha maisha yao, wakijitafutia kipato.
“Ukikaa ndani ya eneo la biashara lenye kodi kubwa unaweza usipate wateja wa kutosha. Lakini hapa barabarani watu wanakuona moja kwa moja,” amesema Juma, muuzaji wa vifaa vya simu katika barabara ya Mandela.
Hata hivyo, Juma anakiri kuwa faida hiyo inaambatana na changamoto nyingi.
“Ni kweli tunapata wateja wengi, lakini hatuwezi kupingana na ukweli kwamba tuko karibu na hatari. Ukiteleza kidogo unaweza kugongwa na gari au bodaboda hizi zinazokatisha bila tahadhari,” amesema Juma.
Kwa wafanyabiashara hawa, ajali si jambo la kusikia tu kwenye vyombo vya habari, wanakiri kuwa sekunde zinaweza kubadili maisha kama ambavyo wamewahi kushuhudia kwa wenzao wenzao wakiumia au kupoteza maisha.
Sadick Ngajime ambaye ni muuzaji wa spea za magari amesema mwaka uliopita alishuhudia mwenzake akigongwa na gari wakati akijaribu kumfuata mteja aliyekuwa ndani ya gari.
Elizabeth Edward
“Alikuwa anauza flash na stendi za simu, kama kawaida alimfuata mteja taa zikawa zimeruhusiwa, wakati anajaribu kumkimbiza, gari lilipogeuka ghafla pale kwenye kona likampiga. Tangu siku hiyo kila nikisikia breki kali huwa nashtuka,” amesema Ngajime.
Amesema baadhi ya wafanyabiashara hulazimika kukimbia pembeni ya barabara ili kuepuka magari yanapopoteza mwelekeo.
“Tatizo ni kwamba tunafanya kazi sehemu ambayo haijatengwa kwa ajili ya biashara. Lakini hatuna sehemu nyingine rahisi kupata wateja,” amesema.
Wanawake wanaofanya biashara katika maeneo hayo wamekuwa kwenye mazingira magumu zaidi, mbali na kukimbiza wateja walio kwenye magari yanayotembea.
Baadhi yao huenda na watoto wadogo mgongoni kwenye maeneo ya biashara, hali inayoongeza changamoto za usalama.
Mtaalamu wa masuala ya jinsia, Anna Mushi amesema wanawake wengi huingia kwenye biashara za barabarani si kwa sababu wanapenda mazingira hayo, bali ni kutokana na ukosefu wa mitaji ya kuendesha biashara rasmi.
“Wanawake wengi wanaotafuta kipato huanza na biashara ndogo kwa sababu haihitaji mtaji mkubwa. Tatizo linakuja pale ambapo mazingira ya kazi yanakuwa tishio kwa afya na usalama wao,” amesema Anna.
Mtaalamu huyo amesema suluhisho linahitaji kuangalia mahitaji halisi ya wafanyabiashara hao badala ya kuwaondoa bila kuwapatia njia mbadala.
Tishio zaidi ya ajali
Mbali na hatari ya kugongwa, wafanyabiashara hao wanakabiliwa na changamoto nyingine ikiwemo kupoteza bidhaa wakati wa oparesheni za kuwaondoa maeneo yasiyoruhusiwa.
Baadhi yao wamesema wakati mwingine hulazimika kukimbia wanapoona askari au maofisa wa mamlaka wakifika, jambo linaloweza kusababisha ajali.
“Mara nyingine unakimbia na mzigo kichwani. Unaweza kujikwaa, kugongwa au kuumia. Lakini unafanya hivyo kwa sababu bidhaa ndiyo maisha yako,” amesema Hamisi Mwinyi, muuza viatu.
Mtaalamu wa mipango miji, Joseph Mhando, amesema uwepo wa biashara barabarani unaonyesha pengo kati ya mahitaji ya wananchi na mipango ya matumizi ya ardhi mijini.
“Watu wanahitaji maeneo ya biashara yenye gharama nafuu. Kama hayapo, watajitafutia maeneo ambayo yana wateja wengi hata kama ni hatari,” amesema Mhando.
Mtaalamu wa usafirishaji Daniel Kweka amesema tatizo la biashara za barabarani linahitaji suluhisho la muda mrefu linalounganisha usalama, ajira na mahitaji ya wananchi.
Kweka amesema maeneo mengi yenye wafanyabiashara hao hayana miundombinu inayolinda watembea kwa miguu wala wafanyabiashara.
“Unapokuwa na mtu anauza bidhaa sentimita chache kutoka kwenye magari yanayopita kwa kasi, tayari una mazingira hatarishi. Lazima mipango ya miji izingatie shughuli za kiuchumi zinazofanyika,” amesema Kweka.
Mtaalamu huyo ameshauri kuwepo kwa maeneo maalumu ya biashara yenye miundombinu salama karibu na maeneo yenye wateja.