
Aprili 3, 2026, gazeti la New York Times, lilichapisha makala yenye kichwa, “Wealthy Donors Are Hiding Political Money in Secretive Nonprofits” ikimaanisha; “Wafadhili Matajiri Wanaficha Fedha za Kisiasa kwenye Asasi zenye Usiri.” Kwamba asasi za kiraia zenye usiri, hutumika kupitisha fedha za kisiasa.
Katika makala hiyo, waandishi Theodore Schleifer na Steven Rich, waliandika kuwa kupitia mtindo wa upitishaji fedha kwenye asasi za siri, mabilionea wanaofahamika kuwa wafuasi wa Chama cha Democratic, Bill Gates na Michael Bloomberg, huwezi kuwaona popote wanapotaka kucheza siasa kwa kuchangia chama chao.
Kwa sheria za Marekani, ni kosa michango ya hisani kutumika kwenye kampeni za kisiasa. Kuzunguka kizingiti hicho, wafadhili matajiri hutumia njia tofauti. Wanapitisha fedha kwenye asasi za kiraia ambazo huficha taarifa zao, kisha vyama vya siasa hupokea michango ya kifedha kutoka asasi za kiraia, ambazo huzitumia kwenye kampeni.
Marekani wameweka sheria ngumu kwa matajiri kuchangia fedha moja kwa moja. Hofu ni matajiri kuteka dola kupitia ushawishi wa kifedha kwa mgombea ambaye wanaweza kumfanya ashinde. Ni kwa sababu Marekani wana uzoefu wa matukio ya fedha za siasa. Tukio la kwanza ni la miaka 198 iliyopita. Karne mbili kasoro miaka miwili.
Uchaguzi wa Rais wa Marekani mwaka 1828, ulimuingiza madarakani Andrew Jackson, mwanasiasa wa kwanza nchini humo kushinda urais bila kuwa na utajiri wa mali, wala hakutokea familia tajiri. Ilibidi Jackson akusanye michango kumwezesha kufanya kampeni zake. Ushindi wake uliibua hofu ya wenye fedha “kumteka”. Mwaka 1867, kampeni ya kudhibiti michango ya kifedha kwenye siasa ilianzishwa.
Mwaka 1883, Sheria ya Mabadiliko ya Utumishi wa Umma ilipitishwa. Lengo lilikuwa kudhibiti watu kunufaika na ajira serikalini baada ya kumsaidia mwanasiasa kushinda urais.
Pamoja na hivyo, Uchaguzi wa Urais Marekani mwaka 1896 uliowakutanisha William McKinley ambaye alishinda dhidi ya William Bryan, uliandika historia ya kugubikwa na vitendo vya rushwa, maana matajiri walimwaga fedha nyingi kwa wagombea.
Uchaguzi wa Urais wa Marekani mwaka 1904, ulikumbwa pia na kashfa kubwa ya fedha za mashirika makubwa ya kibiashara. Kutokana na kashfa hiyo kutikisa nchi, aliyekuwa Seneta wa Carolina Kusini, Benjamin Tillman alipeleka hoja kwenye bunge, Congress, ya kuzuia fedha za kampuni za wafanyabiashara kwenye kampeni, kisha mwaka 1907, Rais Theodore Roosevelt alisani kuwa sheria. Mwaka 1910, ilipitishwa sheria inayotaka uwazi kwenye fedha za uchaguzi.
UK nayo ina changamoto zake za fedha na siasa. Mwaka 2001, taa nyekundu iliwaka baada ya kubainika kuwa vyama vya Conservative na Labour, vilikusanya Pauni 31.6 milioni (Sh108 bilioni). Hatari iliyoonekana ni asilimia 55 ya fedha hizo, yaani pauni milioni 17 (Sh60 bilioni), zilitoka kwa wafanyabiashara tisa tu.
Afrika Kusini, mabilionea Patrice Motsepe, Martin Moshal na Nicky Oppenheimer walitangazwa katika matamko ya vyama vya siasa, kwamba walichangia fedha kwenye robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/2024. Mazingira ya kisiasa Afrika Kusini yanaruhusu wafanyabiashara kuchangia vyama fedha kwa uwazi. Tanzania, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, Chama cha Mapinduzi (CCM), kilikusanya michango ya fedha taslimu na ahadi ya takriban Sh90 bilioni, kwa ajili ya kampeni na ujenzi wa ofisi mpya za chama. Wafanyabiashara mbalimbali walijitangaza hadharani na kiasi walichokitoa. Shughuli ya uchangishaji fedha ilifanyika Mlimani City, Dar es Salaam.
Michango ya wafanyabiashara hao kwa CCM ilibeba tafsiri moja kubwa ya kuingia kwenye kitabu kizuri cha chama hicho. Ni dhana ipo kwa muda mrefu kuwa wafanyabiashara kuichangia CCM, ama kwa siri, au hadharani, ni halali. Dhambi ni kuchangia vyama vya upinzani.
Ilihitaji wafanyabiashara matajiri wenye uthubutu kama Mustafa Sabodo, ambaye alikuwa akiichangia Chadema waziwazi. Sabodo angeitisha mkutano na waandishi wa habari, halafu angetangaza kuichangia Chadema Sh100 milioni. Tanzania haijapata kutokea wafanyabiashara kuwa huru kujulikana kuwa wanachangia fedha vyama vya upinzani.
Ipo dhana kuwa wafanyabiashara hukimbilia kuchangia CCM ili kusaka ulinzi wa biashara zao. Maana ndiyo chama kinachoongoza dola. Upande wa pili wa dhana hiyo ni unaeleza kuwa, wafanyabiashara huogopa kujulikana wanachangia fedha vyama vya upinzani kwa kuhofia kupata matatizo ya kibiashara.
Mwaka 1999, mfanyabiashara mmoja maarufu Tanzania, alipata matatizo kwa bidhaa zake alizoingiza nchini, kuonekana hazikuwa na ubora, hivyo kuteketezwa. Dhana iliyoenea mtaani ni kwamba bidhaa hizo hazikuwa mbovu, isipokuwa mfanyabiashara huyo alikomolewa kwa sababu alikifadhili Chama cha Wananchi (CUF).
Iwe kwa ukweli au uvumi wa mitaani, hofu ni kwamba wafanyabiashara wanaogopa kuchangia vyama vya upinzani kwa sababu wanaweza kufilisiwa, au kupewa misukosuko ya kodi. Ni kwa sababu hiyo, wafanyabiashara wa Tanzania hujitahidi kutoa fedha kwa mkono mmoja kwenda vyama au marafiki zao wa upande wa upinzani, pasipo mkono wa pili kujua.
Hivi karibuni, kumeibuka shutuma zenye kubeba madai kuwa zilianzia kwenye mkutano wa Kamati Kuu Chadema, uliofanyika Kigoma, Juni 29, 2026. Inadaiwa kuwa ndani ya Kamati Kuu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, John Heche alituhumiwa kutumia vibaya fedha za michango ya wafanyabiashara. Kwamba fedha hizo amezitumia bila uwazi, na huwa hafikishi kwenye chama. Inadaiwa kuwa majina ya wafanyabiashara yalitajwa.
Hatari ni kuwa majina hayo yameanza kujadiliwa kwenye uso wa jamii. Pamoja na Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika, kutokeza na kufafanua baadhi ya tuhuma, ukweli ni kwamba kitendo cha majina ya wafanyabiashara kutajwa, iwe kweli, au wanasingiziwa, itakimbiza wengi. Wataogopa kuchangia Chadema, maana hakuna siri, na fedha hazitumiki kwa malengo yenye kutarajiwa.