Chanzo cha picha, Haika Lawere
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4
Kwa mfanyabiashara Haika Lawere, umiliki wa mali kwa mwanamke si suala la hanasa, bali ni haki ya msingi ambayo kila mwanamke anapaswa kuwa nayo.
“Mwanamke yoyote, kuanzia miaka kumi na nane hadi mia moja na ishirini, miliki mali, miliki biashara, miliki nyumba za biashara, miliki ardhi, miliki viwanja, miliki mifugo, miliki mashamba, miliki akaunti za benki, uwe na akaunti zako, uwe na akiba, kuwa na hisa, kuwa na bonds au dhamana za uwekezaji,” anasema Haika.
Anaongeza kuwa umiliki huo haupaswi kuonekana kama changamoto ndani ya ndoa au mahusiano, bali kama sehemu ya kujenga familia yenye nguvu kiuchumi.
“Hiyo ni haki ya kimsingi kwa binadamu yoyote, na mwanamke pia kama binadamu kamili ana haki ya kumiliki hivyo vitu.”
Kwa Haika, mwanamke kuwa na mali zake binafsi pia kunaweza kuwa kinga kwa familia nzima, ikiwemo mwanaume.
“Kwasababu pia tunapoongea kuhusu watu kuwa na mali zao binafsi inamlinda hata mwanaume mwenyewe ambaye anafanya kazi kwa jasho,” Haika anasema.
Anasema wanandoa wanapaswa kufurahia mafanikio ya wenzao badala ya kuyaona kama tishio.
“Ni vizuri wanaume wakafurahi mwenza wao akileta pesa nyingi… kwasababu akitengeneza bilioni moja, atasaidia uchumi wa ile familia.”
“Ndoa ni kubebana”
Chanzo cha picha, Haika Lawere
Haika, ambaye alikuwa kwenye ndoa kwa takribani miaka 20, anasema jambo kubwa alilojifunza ni umuhimu wa ushirikiano na kuwa mfumo wa msaada kwa mwenza.
“Kitu ambacho nimejifunza ni kwamba katika ndoa, mkifanya kazi pamoja mnakwenda mbali sana.”
Anasema uwazi, kuaminiana na upendo ni msingi muhimu wa safari ya watu wawili.
“Kuna ile akiba yani kwamba mimi ninapokuwa nimechoka kuna mwenzangu ananisaidia kubeba ule mzigo. Mimi ninapokuwa nimepata nguvu, mwenzangu labda ameshuka.”
Kwa mtazamo wake, suala la uchumi ni moja ya nguzo muhimu ndani ya ndoa.
“Mimi kitu namba moja ninachoona ni cha muhimu sana kwenye ndoa ni suala la uchumi, kushirikiana pamoja ni kitu namba moja.”
Anasema maisha yana mabadiliko na mtu anaweza kuhitaji msaada wa mwenza wake wakati wowote.
Kuanzisha biashara: “Usifikirie sana mpaka ukashindwa kuanza.”
Chanzo cha picha, Haika Lawere
Kwa wanawake wanaotamani kuingia kwenye biashara lakini wanaogopa kuanza, Haika anasema hatua ya kwanza ni kuchukua hatua.
“Mimi nasema hivi ukitaka kuogelea, wewe usijali nyuzi joto ya maji kama ni baridi, moto au nini, yani wewe vua nguo tumbukia, alafu utajua mbele kwa mbele.”
Anasema watu wengi hutumia muda mwingi kufikiria badala ya kuanza.
“Biashara ingia kwanza, alafu jifunze hivyo vitu vya biashara ndani yake, usikubali kutumia muda mwingi kufikiria hadi ukashindwa au ukachelewa kuanza.”
Anashauri wanawake kuanza hata kwa kiwango kidogo, hasa kupitia teknolojia na mitandao ya kijamii.
“Mimi huwa nawaambiaga biashara anza kwanza kwenye mitandao kwaajili ya kujenga soko, cha pili kujijengea uwezo.”
Kwa Haika, biashara ni safari ya kujifunza ambayo inahitaji uvumilivu, maarifa na uwezo wa kubadilika.
“Mimi sipendi kukaa nipewe”
Haika anasema tangu akiwa mdogo amekuwa na hamu ya kujenga vitu na kuwa mtu wa kutoa.
“Mimi sitopenda kukaa nipewe, hicho kitu kimeniathiri mpaka leo hii kiasi kwamba ninapenda kuwa kama mtu anayetoa kwa wengine”
Anaeleza kuwa anafurahia kuona matokeo ya kazi yake.
“Mimi ni mtu ambaye ninapenda kuona kazi za mikono yangu. Nikiona leo nimepata hela nimepambana nimenunua nyumba, nimepambana nimejenga ukumbi, nimepambana hapa nimejenga mgahawa.. yani mimi ni mtu ambaye ninapenda kuzaa vitu,”
Kwa mujibu wake, uwezo wa wanawake ni mkubwa zaidi ya wanavyoweza kufikiria.
“Kuna wanawake ambao huenda wakawa wana uwezo mkubwa sana, na ukiwaruhusu wakafanya biashara wakaenda Kariakoo, China, Uturuki, watafanya biashara kiasi cha kwamba utashangaa ukubwa na uwezo walio nao.”
Ajira na biashara pembeni
Haika pia anasisitiza umuhimu wa watu walioajiriwa kuwa na vyanzo vingine vya mapato.
Anasema ajira pekee inaweza kuwa ni changamoto kwasababu hakuna kazi iliyo ya milele.
“Kazi sio za milele, hata biashara sio za milele.”
Anashauri watu kuanza biashara wakiwa bado wana ajira badala ya kuacha kazi ghafla bila mpango.
“Usiache tu ghafla kwasababu mwajiri kakutukana, kakugombeza, au umekasirika.”
Anasema wengi wanaofanikiwa kwenye biashara baada ya kuacha ajira walijipanga mapema na walijenga biashara zao taratibu.
Malezi: Kuwajenga watoto wanaoweza kuendana na dunia ya sasa
Chanzo cha picha, Haika Lawere
Mbali na biashara, Haika amezungumzia pia safari yake ya malezi na namna yeye na aliyekuwa mwenza wake walivyowalea watoto wao.
Anasema lengo lake lilikuwa kuwajenga watoto wenye uwezo wa kuendana na dunia ya sasa.
“Mimi kwenye watoto nilitaka sana nilee watoto wenye uwezo wa kushindana na kuishi katika mazingira ya sasa popote duniani, yani kwamba akienda Marekani, akienda Uingereza, akienda nchi yoyote ile awe tu anaweza kujichanganya na watu wa hapo”
Anasema aliwekeza katika elimu ya ziada nje ya darasani, ikiwemo midahalo, mashindano mbalimbali, michezo na shughuli za kijamii.
“Nilikuwa nafanya vile vitu ambavyo vipo nje ya darasani.”
Pia anaeleza umuhimu wa kuwapa watoto uzoefu wa kusafiri na kukutana na tamaduni tofauti.
“Kadri unavyoweza, mfanye mtoto aone dunia nje ya masuala ya masomo shuleni, kwasababu dunia ya leo inataka mtoto ambaye ana utandawazi.”
Kwa Haika, uzoefu huo uliwasaidia watoto wake kujiamini, kuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza na mtazamo mpana kuhusu dunia.
“Kinacho tukwamisha wanawake ni hofu yetu”
Akizungumza kuhusu wanawake kwa ujumla, Haika anasema uwezo upo, lakini mara nyingi kinachozuia ni hofu.
“Sisi wanawake tuna nguvu kubwa sana ya kufanya chochote. Kinacho tukwamisha ni mitazamo yetu hasi, na wasiwasi na uoga wetu,” Haika anasema.
Anaamini wanawake wakipata maarifa, msaada na nafasi ya kujaribu, wanaweza kujenga biashara kubwa na kufikia malengo yao.
“Cha kwanza utatafuta maarifa… kisha baada ya muda ukishapata maarifa, unaanza kwenye kiwango kidogo, kisha uone maono ya mtazamo wa biashara yako kwa baadaye alafu endelea mbele polepole.”