Dodoma. Mtanzania Gloria Majule ameibuka kidedea na kubamba katika mabango ya miji mikubwa nchini Marekani ikiwemo New York baada ya kushinda tuzo katika sinema yake ya Malaria.
Kwenye sinema hiyo, ameelezea kwa upana kuhusu Malaria na jinsi ya kukabiliana nayo akitumia wahusika wakuu na mifano kwa nchi zinazoendelea na mara nyingi amekuwa akijikita katika simulizi za maisha ya watu weusi.
Katika picha za mabango nchini Marekani, jina la Gloria Majule linaonekana kwenye maeneo maafuru na barabara kuu kukiwa na maandishi ya sinema hiyo kwenye ushindi wake wa mwaka 2025/26.
Gloria ni mtoto wa mbunge wa viti maalum Mkoa wa Dodoma, Dk Neema Majule ambaye ameeleza kuupokea ushindi wa mwanaye kwa furaha, akisema imemchukua muda kuzifikia ndoto hizo kwani alianza kupambana tangu akiwa mwanafunzi wa chuo.
Wasifu wa Gloria ambao umethibitishwa na mama yake mzazi, alihitimu shahada ya juu (Summa cum laude) kutoka Chuo Kikuu cha Cornell alikosomea Sanaa (BA), akibobea katika sanaa za maonyesho na vyombo vya habari katika lugha ya Kihispania.
Anatajwa kuwa mwanamke wa kwanza wa Kiafrika kupata Shahada ya Uzamili ya Sanaa (MFA) katika uandishi wa tamthilia kutoka shule kuu ya sanaa ya kuigiza ya Yale (Yale School Of Drama).
Katika wasifu huo, amefikia hatua ya fainali mara tatu katika tuzo za O’Neill Blackburn huku akiwa ni mshirikia wa mpango wa MacDowell (MacDowell Fellow).
Kwa mujibu wa maelezo yake, amekuwa akipokea maombi ya kufanya kazi kutoka Audible, Milwaukee Reportory Theater, Atlantic Theater Company na Chuo Kikuu cha Princeton/The Civilians huku akishiriki katika programu za makazi ya kisanii huko Yaddo Art Omi, The New Harmony Project na New York Stage and Film.
Miongoni mwa tamthilia alizowahi kushiriki ni My Father Was Short in Back of Head (ilifika fainali katika tuzo ya Relentless), Culture Shock (alikuwa mshindi wa tuzo ya Leah Ryan), Mala Aria (alikuwa wa tuzo ya Premiere Stages), Uhuru na Fifteen Hundred.
Kwenye tamthilia ya Uhuru inamhusu Mshale, mwongoza watalii wa Mlima Kilimanjaro mwenye ndoto ya kumuoa mzungu na kuhamia nchi za Magharibi huku akiwaonyesha wahusika wanaokabiliana na masuala ya ukoloni na utambulisho.
Kwa sasa mtunzi na mshindi huyo anafanya kazi kama Profesa wa Uandishi wa Tamthilia katika Chuo Kikuu cha Sanaa cha Cornish (Cornish College of the Arts).