
SIMBA imewaaga nyota wake saba ikianza mkakati wa kusuka kikosi chake kwa msimu ujao wa 2026-2027.
Taarifa iliyotolewa na Simba leo Julai 16, 2026, ni kwamba klabu hiyo imewaacha wachezaji wanne wa kigeni na watatu wazawa kwenye orodha hiyo.
Wachezaji wazawa walioachwa ni viungo Edwin Balua, Awesu Awesu na Omari Omari ambao wote hawakuwa sehemu ya kikosi hicho kwenye nusu ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu Bara 2025-2026.
Viungo hao walisajiliwa wakati kikosi hicho kinafundishwa na kocha Fadlu Davids, kisha kukosa nafasi ya kufanya makubwa.
Kwa upande wa wale wa kigeni, Simba imemuaga kipa Moussa Camara anayekaribia kusaini nchini Ufaransa, beki Chamou Karaboue aliyekwenda Iraq.
Wengine ni viungo Naby Camara aliyemaliza na Simba ya msimu uliopita na Mzambia Joshua Mutale.
Taarifa hiyo imeshtua kwa kukosekana mshambuliaji Jonathan Sowah ambaye alikuwa kwenye mgogoro na klabu hiyo, huku ikielezwa kwamba raia huyo wa Ghana anarejea Singida Black Stars ambayo alitokea huko wakati anatua Simba msimu wa 2025-2026.