
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), wawekezaji wanasema bado kuna vikwazo vinavyoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi hiyo.
Wanataja kutokuwa na uhakika wa kurejesha mitaji, mabadiliko ya sera, mifumo isiyoeleweka na changamoto za upatikanaji wa fedha kuwa miongoni mwa mambo yanayowafanya kuwa na hofu ya kuwekeza.
Kwa upande wake, Serikali inasema tayari imeshafanya jambo na kutatua changamoto zote za kisheria, kisera na mikataba ili kuhakikisha inalinda mitaji ya wawekezaji na kuwavutia zaidi kuingia katika ubia.
Juni 23, 2026 Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alitangaza miradi ya barabara ambayo Serikali inataka kuitekeleza kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Miradi hiyo ni ya Barabara ya Morogoro-Dodoma yenye urefu wa kilomita 260 itakayojengwa kwa njia nne.
Nyingine ni Barabara ya Chalinze-Segera-Tanga, Dar es Salaam-Kibaha yenye urefu wa kilomita 42 na Handeni-Kiberashi-Chemba-Kwamtoro-Singida yenye kilomita 384.
Mradi mwingine ni wa barabara ya mchepuko katika eneo la Mkina Kitonga mkoani Iringa pamoja na barabara ya haraka kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kutumia sekta binafsi katika ujenzi na uendeshaji wa miradi mikubwa badala ya kutegemea fedha za umma pekee.
Mwelekeo huo unaendana na hali ya Afrika, ambako mahitaji ya uwekezaji wa miundombinu yamekuwa makubwa kuliko uwezo wa Serikali nyingi.
Ripoti ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ya mwaka 2024 inaonesha Bara la Afrika linahitaji kati ya Dola 130 bilioni za Marekani hadi bilioni 170 (takribani Sh337 trilioni hadi Sh437 trilioni) kila mwaka kwa miundombinu.
Hali ikiwa hivyo, bado kuna pengo la ufadhili ambalo katika ripoti inaelezwa linakadiriwa kuwa kati ya Dola 68 bilioni hadi Dola 108 bilioni kwa mwaka (takribani Sh176.8 trilioni hadi Sh280.8 tilioni).
Kutokana na hali hiyo, nchi nyingi zimekuwa zikitegemea ubia wa Serikali na sekta binafsi kuziba pengo hilo.
Hata hivyo, wadau wanasema mfumo huo hautafanikiwa bila kushughulikia hofu zinazowafanya wawekezaji kusita kuingia kwenye miradi ya muda mrefu.
Ulinzi wa uwekezaji
Mhandisi kutoka kampuni binafsi ya ujenzi, Flavius Matata anasema sekta binafsi iko tayari kushirikiana na Serikali, lakini inahitaji uhakika wa ulinzi wa uwekezaji wake.
Anasema kampuni nyingi zina uwezo wa kifedha na kitaalamu kushiriki katika miradi mikubwa, lakini hofu kubwa ni namna masilahi yao yatakavyolindwa.
Matata anasema miradi ya PPP hujengwa kwa makubaliano ya muda mrefu yanayohusisha mgawanyo wa mapato kati ya Serikali na mwekezaji.
Anasema mikataba huweka wazi namna kila upande utakavyonufaika baada ya mradi kuanza kuzalisha mapato.
Hata hivyo, anasema mazingira ya utekelezaji yanaweza kubadilika na kusababisha mapato kuwa tofauti na makadirio ya awali.
“Unaweza kukubaliana sekta binafsi ichukue asilimia 70 ya faida na Serikali asilimia 30, lakini baadaye hali ikawa tofauti na hesabu za mwanzo,” anasema.
Matata anasema mabadiliko hayo yanaweza kusababisha mradi kushindwa kurejesha gharama za uwekezaji ndani ya muda uliokubaliwa.
Ni mtazamo wake kuwa, mikataba inapaswa kuweka wazi namna ya kulinda masilahi ya wawekezaji endapo kutatokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi.
Mabadiliko ya kisiasa
Mbali na masuala ya kifedha, anasema kutotabirika kwa mazingira ya kisiasa ni sababu nyingine inayowafanya wawekezaji kuwa na hofu ya kuwekeza.
Anasema mwekezaji anaweza kusaini mkataba na Serikali ya awamu moja, lakini nyingine ikaibuka na kutaka kubadili masharti yaliyokubaliwa.
Kwa maoni yake, hali hiyo inaweza kusababisha hasara kubwa kwa kampuni iliyokwishawekeza fedha nyingi.
Anasisitiza kuwa, mikataba lazima iwe na kinga zinazolinda pande zote iwapo kutatokea mabadiliko ya kisiasa.
Vilevile, anasema uhakika wa kisiasa na mikataba imara unaweza kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya PPP.
Mfumo ni kikwazo
Mkurugenzi Mtendaji wa Aquifer Construction Limited, Milton Nyerere anasema PPP si jambo jipya nchini, lakini changamoto kubwa imekuwa mifumo na taratibu kutokuwa wazi kwa wawekezaji.
Anasema miradi hiyo huhitaji kampuni binafsi kutafuta fedha na kuwekeza kabla ya kuanza kurejesha gharama zake.
Ni mtazamo wake kuwa, changamoto kubwa kwa kampuni za ndani siyo uwezo wa kujenga, bali kupata fedha na washirika wa kugharimia miradi mikubwa.
“Shida kubwa kwetu ni kupata taasisi au wawekezaji wanaoweza kutoa fedha za kutekeleza miradi mikubwa,” anasema.
Anasema wawekezaji wanahitaji kuona mfumo unaoeleweka kabla ya kuamua kuingiza mitaji yao.
Ripoti ya Benki ya Dunia inaonesha mwaka 2023 nchi za kipato cha chini na cha kati zilivutia uwekezaji binafsi wa Dola 86 bilioni (takribani Sh223.6 trilioni) kupitia miradi 322 ya miundombinu.
Ripoti hiyo inaeleza wawekezaji huvutiwa zaidi na nchi zenye mifumo wazi, mikataba inayotekelezeka na mazingira yanayotabirika.
Nyerere anasema aliwahi kufanya mazungumzo na wawekezaji wa Korea kuhusu miradi ya miundombinu, lakini walitaka kuona mfumo unaoeleza uwekezaji na namna ya kupata faida.
Anasema pamoja na Serikali kufanya mijadala kuhusu PPP, bado kuna haja ya kuweka utaratibu unaoeleweka zaidi kwa wawekezaji.
“Bila mfumo huo, inabaki kuwa ndoto zaidi kuliko uhalisia,” anasema.
Changamoto ya kifedha
Nyerere anasema upatikanaji wa fedha za miradi mikubwa bado ni changamoto kwa kuwa benki nyingi za ndani hutegemea dhamana za mali kuliko uwezo wa mradi kuzalisha mapato.
Anasema miradi ya PPP inahitaji mfumo wa ufadhili unaozingatia uwezo wa mradi kulipa gharama zake baada ya kuanza kufanya kazi.
Anasema bado kuna upungufu wa utaalamu katika eneo hilo, jambo linalohitaji muda kujenga uwezo wa taasisi za fedha kushiriki katika miradi mikubwa.
Mhandisi kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Estim, Fred Nyenga anasema ingawa dhana ya PPP imezungumzwa kwa muda mrefu, utekelezaji wake nchini bado ni jambo jipya.
Anasema hali hiyo inawafanya wawekezaji kujiuliza kama wataweza kurejesha mitaji yao, hasa kwa kuwa faida ya miradi hiyo hupatikana baada ya muda mrefu.
“Wawekezaji wanaangalia uhakika wa fedha zao. Najenga na naendesha ili nirudishe fedha yangu. Nina uhakika gani miaka 10 au 15 mbele?” anasema.
Mitaji na ujuzi kwa wazawa
Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bandari Kavu Tanzania (CIDAT), Mellek Shange anasema changamoto kubwa kwa wawekezaji wazawa katika PPP ni mitaji na utaalamu.
Anasema miradi mingi ya ubia huhitaji fedha nyingi ambazo wafanyabiashara wengi wa ndani hawawezi kuzifikia.
“Changamoto huwa mara nyingi ni mitaji. Kwenye PPP mitaji inayohitajika ni mikubwa na Watanzania wengi hawana uwezo wa kuifikia,” anasema.
Anasema Serikali inapaswa kuweka mazingira yatakayowawezesha wawekezaji wa ndani kupata mitaji hiyo na kushiriki katika miradi mikubwa.
Mbali na fedha, Shange anasema baadhi ya miradi huhitaji utaalamu maalumu ambao bado ni mdogo nchini.
“PPP inakuja lakini ujuzi bado uko nyuma. Wakati mwingine wataalamu wa ndani hawatoshi au hawapo kabisa,” anasema.
Yanayohitaji kufanyika
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Dk Ludas Mwasomola anasema Serikali inapaswa kujenga mazingira ya uhakika kwa wawekezaji wa muda mrefu.
Anasema sheria na mikataba ya PPP inapaswa kuwa na kinga zinazolinda uwekezaji dhidi ya mabadiliko ya kisiasa.
“Mwekezaji anahitaji kuona mkataba wake ni salama kuliko mabadiliko ya kisiasa,” anasema.
Ni mtazamo wa mchambuzi wa uchumi, Modest Mollel kuwa, changamoto kubwa siyo ukosefu wa miradi, bali mifumo ya kuwezesha sekta binafsi kupata fedha.
Anasema Serikali inaweza kuanzisha mifuko ya dhamana au kushirikiana na taasisi za fedha za kimataifa kupunguza hatari kwa wawekezaji.
“Miradi mingi inakosa fedha kwa sababu hatari zote zinaachwa kwa mwekezaji. Serikali ikibeba sehemu ya hatari, mtaji utapatikana kwa urahisi zaidi,” anasema.
Dk Magdalena Tilungwa mchambuzi wa sera za uchumi anasema benki nyingi bado zinatoa mikopo kwa kuangalia dhamana za mali badala ya uwezo wa mradi kuzalisha mapato.
Anasema kuna haja ya kujenga uwezo wa taasisi za fedha katika ufadhili wa miradi mikubwa na kuziunganisha na masoko ya fedha ya kimataifa.
“Bila mageuzi katika sekta ya fedha, miradi mingi ya PPP itaendelea kuwa mipango mizuri kwenye makaratasi,” anasema.
Inachofanya Serikali
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP Center), David Kafulila anasema baadhi ya hoja za wadau zinatokana na kutokutofautisha miradi ya PPP na ile ya kawaida ya Serikali.
Anasema miradi ya PPP ina taratibu zake tofauti, ambapo inaweza kuanzishwa na Serikali au mwekezaji mwenyewe.
Kafulila anasema msingi wa uamuzi wa utekelezaji wa mradi wowote ni upembuzi yakinifu unaoonesha gharama, manufaa na namna ya utekelezaji.
“Upembuzi yakinifu ndiyo unaotoa majibu kuhusu uhalali wa mradi na namna utakavyotekelezwa,” anasema.
Kafulila anasema miradi ambayo haijaandaliwa na Serikali hupewa nafasi wawekezaji kuandaa mapendekezo yao na kufanya tathmini kabla ya kuanza.
Akijibu hoja ya mifumo kutokuwa wazi, anasema Serikali imeweka sheria, kanuni na taratibu zote za PPP na imekuwa ikitoa elimu kwa wadau.
“Sheria na kanuni zote ziko wazi na zinapatikana. Tumekuwa tukifanya mafunzo na mijadala na sekta binafsi kuongeza uelewa,” anasema.
Kuhusu upatikanaji wa fedha, anaeleza kuwa, sheria inaruhusu Serikali kutoa dhamana, kuchangia mtaji wa mradi na kutoa vivutio vya kikodi kwa wawekezaji.
Anasema hatua hizo zinalenga kusaidia upatikanaji wa mikopo na kuhakikisha miradi mikubwa inatekelezeka.
Akizungumzia hofu ya mabadiliko ya kisiasa, Kafulila anasema sheria imeweka kinga kwa wawekezaji kupitia marekebisho yaliyofanyika mwaka 2023.
“Migogoro ya uwekezaji inaweza kupelekwa kwenye vituo vya kimataifa vya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji,” anasema.
Anasema marekebisho hayo yalilenga kuendana na viwango vya kimataifa na kuongeza imani ya wawekezaji.
“Hata uongozi ukibadilika, kuvunja au kubadilisha mkataba kiholela kunaweza kuigharimu Serikali kwa sababu mwekezaji ana haki ya kufuata taratibu za usuluhishi,” anasema.