Dar es Salaam. Serikali imesema ujenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Reli katika Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ni sehemu ya mradi wa uhuishaji wa reli hiyo unaolenga kuandaa wataalamu watakaohudumia Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, amesema kituo hicho kitaanza kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Tazara watakaoshiriki katika mradi wa uboreshaji wa reli kabla ya kupokea vijana na watu wengine wanaotaka kujifunza taaluma mbalimbali za reli.
Profesa Kahyarara alitoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 17, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Mafunzo na Kituo cha Kudhibiti Uendeshaji wa Reli katika Karakana za Tazara, jijini Dar es Salaam.
Alisema chuo hicho kitapokea wanafunzi kuanzia ngazi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na kitakuwa na warsha pamoja na vifaa vya kisasa vitakavyowezesha mafunzo ya uendeshaji wa treni, matengenezo, uhandisi na mifumo ya ishara za reli.
Alisema kuongezeka kwa mtandao wa Reli ya Kisasa (SGR), Reli ya Mita (MGR) na Tazara kumeongeza mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi, hali iliyosababisha Serikali kuwekeza katika mfumo rasmi wa mafunzo ya kitaalamu.
“Tofauti na zamani ambapo wafanyakazi wengi walijifunza wakiwa kazini, sasa kutakuwa na mfumo rasmi wa mafunzo unaowaandaa wataalamu kabla ya kuingia kwenye ajira,” amesema.
Profesa Kahyarara amesema mtandao wa SGR unatarajiwa kufikia zaidi ya kilomita 4,700 utakapokamilika, huku Tazara ikiendelea kuwa kiungo muhimu cha usafirishaji kati ya Tanzania na nchi za Kusini mwa Afrika kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema Serikali pia inaendelea na mkakati wa kuunganisha nchi jirani zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam kwenye mtandao wa SGR, ikiwamo Burundi, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda na Rwanda zikiendelea na maandalizi ya kujiunga na mtandao huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema kwa zaidi ya miaka 50 Serikali ya China imekuwa ikitoa mafunzo kwa wataalamu wa kiufundi na usimamizi kutoka Tanzania na Zambia.
Amesema mradi wa uhuishaji wa Tazara unatarajiwa kuzalisha maelfu ya ajira na kuongeza mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika uendeshaji na usimamizi wa reli.
“China imeamua kufadhili ujenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Mradi wa Uhuishaji wa Tazara ili kujenga mfumo wa kitaalamu wa mafunzo unaokidhi mahitaji halisi ya mamlaka hiyo na kuandaa wataalamu wazawa wenye ujuzi. Tuko tayari kushirikiana na Tanzania kukifanya kituo hiki kuwa kitovu bora cha elimu ya ufundi wa reli,” amesema.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, Bruno Chinga’andu, alisema kituo hicho kitaimarisha uwezo wa wataalamu wa reli katika nyanja za kiufundi, kiutendaji na kiusimamizi, huku kikichangia uhamishaji wa teknolojia mpya na kuandaa kizazi kipya cha wataalamu.
Alisema Kituo cha Kudhibiti Uendeshaji wa Reli kitasaidia kuratibu safari za treni kwa ufanisi zaidi, kuboresha mawasiliano, kuongeza kasi ya maamuzi na kuimarisha usalama wa huduma za reli.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), Li Chongyang, amesema kampuni hiyo imekamilisha maandalizi muhimu kuhakikisha ujenzi wa miradi hiyo unafanyika kwa viwango vya juu vya ubora.
Amesema Kituo cha Mafunzo kitazalisha wataalamu wazawa wenye ujuzi wa kisasa, huku Kituo cha Kudhibiti Uendeshaji kikitumia mifumo ya kidijitali kuongeza ufanisi wa usimamizi wa reli, kuboresha matengenezo na kuimarisha usalama.
Chongyang amesema CCECC itaendelea kushirikiana na Serikali za Tanzania, Zambia na China pamoja na wadau wengine kuhakikisha mradi wa uhuishaji wa Tazara unakamilika kwa mafanikio.