Zanzibar. Kampuni ya Zanzibar Ferry Development Company Limited (ZF DevCo), kwa kushirikiana na Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), leo limetangaza kuanza kwa hatua ya mwisho ya uhamishaji wa huduma za meli za Roll-on/Roll-off (RoRo) kwenda Kituo Kipya cha Bandari ya Maruhubi.

Zoezi hilo linatarajiwa kuanza Julai 18, 2026 ambapo shughuli zote za mizigo za meli za LCT na RoRo zitafanyika katika Kituo cha Maruhubi, huku huduma zote za abiria, (RoPax) zikitarajiwa kuhamia ifikapo Agosti 2026. Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi wa huduma, kuboresha usalama na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa baharini Zanzibar.

Tangu kuanza kwa majaribio ya operesheni mwezi Aprili 2026 na kuhamishwa kwa shughuli za meli za Landing Craft (LCT) kwa awamu kuanzia tarehe 4 Mei 2026, Kituo cha Maruhubi kimeonyesha mafanikio makubwa katika kuongeza ufanisi wa huduma. Muda wa kuhudumia meli umepungua kwa takribani asilimia 70 ikilinganishwa na Kituo cha Kivuko cha Malindi, huku maboresho yote yaliyobainika wakati wa majaribio yakitekelezwa kwa mafanikio.

Kuanzia Julai 18, 2026, shughuli zote za mizigo zinazohusisha meli za LCT na RoRo zitafanyika katika Kituo cha Bandari ya Maruhubi pekee.

Wakati huo huo, abiria wa meli za RoRo wataendelea kupanda na kushuka kupitia Kituo cha bandari ya Malindi wakati maandalizi ya mwisho ya miundombinu ya abiria katika Kituo cha Maruhubi yakikamilishwa.

Inatarajiwa kuwa ifikapo Agosti 2026, huduma zote za abiria, magari na mizigo zitahamia Maruhubi, na hivyo kukamilisha uhamishaji wa huduma zote za RoRo na RoPax.

Kituo cha Bandari ya Maruhubi kimejengwa kwa viwango vya kisasa ili kuongeza ufanisi wa huduma, usalama na kutoa mazingira bora kwa abiria, waendeshaji wa vyombo na wafanyabiashara.

Mradi huu unaunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ya kuimarisha miundombinu ya usafiri wa bandari, kukuza biashara na utalii.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ZF DevCo alisema:

“Uhamishaji wa shughuli za RoRo kwenda Maruhubi ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za usafiri wa baharini Zanzibar. Hatua hii itapunguza msongamano katika Kituo cha Malindi na kutoa nafasi ya kuboresha miundombinu ya barabara na uwezo wa kituo hicho. Tunawashukuru ZPC, ZMA, SHIPCO, waendeshaji wa vyombo, taasisi za Serikali na wadau wote kwa ushirikiano wao katika kufanikisha uhamisho huu.”

“Tunawakaribisha wadau wote wa sekta ya usafiri wa baharini, wafanyabiashara, waingizaji na wasafirishaji wa mizigo kutumia kikamilifu Kituo cha bandari ya Maruhubi ili kufanikisha azma yetu ya kuendelea kuifungua Zanzibar kiuchumi.”

ZF DevCo na ZPC zinaendelea kushirikiana kuhakikisha mpango huu unafanyika kwa usalama na ufanisi. Wadau wanashauriwa kufuatilia taarifa rasmi kuhusu ratiba za safari, njia za kuingia kituoni na taratibu mpya za matumizi ya Kituo cha Maruhubi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *