
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, serikali ya Uholanzi imeamua kupiga marufuku uingizaji, ununuzi na uuzaji wa bidhaa zinazozalishwa katika maeneo ya vitongozi haramu vya walowezi wa utawala wa Kizayuni.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya msimamo wa Uholanzi wa kutotambua uhalali wa vitongoji vilivyojengwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kwa kuzingatia sheria za kimataifa na maamuzi ya Umoja wa Mataifa.
Hatua hiyo inalenga kuzuia aina yoyote ya uungaji mkono kwa makazi hayo, ambayo ujenzi wake unakiuka sheria za kimataifa.
Wiki iliyopita, serikali ya Ubelgiji pia ilichukua hatua kama hiyo kwa kupiga marufuku bidhaa zinazotoka katika makazi hayo.
Kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ujenzi na upanuzi wa makazi ya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi ni kinyume cha sheria za kimataifa. Hivyo, uzalishaji na biashara ya bidhaa zinazotoka katika maeneo hayo unachukuliwa kuwa ni ukiukaji wa sheria na umepigwa marufuku.
Wakulima wa Israel wameonya kuhusu “kuporomoka kwa mauzo ya nje ya bidhaa za kilimo kufuatia kuongezeka kwa kampeni za kimataifa za kususia bidhaa za Israel kutokana na vita vya Gaza.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, maduka makubwa katika nchi kadhaa za Ulaya yameacha kuuza bidhaa za Israel ili kujibu ghadhabu za wanunuzi za bidhaa hizo kutokana na vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza.