SEKTA ya utalii nchini Tanzania inaendelea kuonesha mafanikio makubwa ya ongezeko la idadi ya watalii na makusanyo ya mapato yanayoendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, jambo ambalo linaifanya nchi kuimarisha nafasi yake ikiwa ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazokua katika sekta ya utalii.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonesha kuwa mwaka 2025 Tanzania ilifanikiwa kupokea watalii milioni 5.94, kutoka milioni 5.36 mwaka 2024 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 10. Katika ongezeko hili, watalii wa kimataifa walifikia milioni 2.29 huku utalii wa ndani ukiendelea kukua kwa kasi na makadirio ya lengo la serikali kufikisha watalii milioni nane ifikapo 2030 kupitia uwekezaji katika miundombinu, matangazo ya vivutio na kuendelea kuboresha huduma za utalii.

Hata hivyo sekta ya utalii imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi kwa ongezeko la mapato ya fedha za kigeni, kuchochea uwekezaji na kutoa ajira katika shughuli zinazohusiana na utalii. Vivutio vya asili kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, eneo la Hifadhi la Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na fukwe za Zanzibar vinaendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya utalii duniani. SOMA: UN yaitaja Tanzania kinara ongezeko la watalii

Kadhalika, Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii ( UN Tourism) limethibitisha kuwa idadi ya watalii walioingia barani Afrika iliongezeka kwa asilimia nne katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, huku Afrika Kaskazini ikiendelea kuongoza kwa kasi ya ukuaji kutokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, usafiri wa anga na kampeni za kutangaza vivutio vya utalii.

Miongoni mwa mataifa yanayoongoza Afrika ni Morocco, ambayo imeendelea kushika nafasi ya juu kwa idadi ya watalii. Mwaka 2025 nchi hiyo ilipokea karibu watalii milioni 20 na sasa inalenga kufikisha milioni 26 ifikapo mwaka 2030. Mafanikio hayo yanachangiwa na upanuzi wa viwanja vya ndege, ongezeko la safari za ndege kutoka masoko makubwa ya dunia pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya utalii kuelekea Kombe la Dunia la mwaka 2030.

Nchi nyingine Misri ambayo imeendelea kufanya vizuri baada ya kupokea takribani watalii milioni 19 mwaka 2025. Serikali ya nchi hiyo imewekeza katika kuboresha huduma za utalii, kuimarisha usalama wa wageni na kuendeleza vivutio vya kihistoria kama Piramidi za Giza, Luxor na Jumba la Makumbusho la Grand Egyptian. Lengo lake ni kufikisha watalii milioni 30 kwa mwaka ifikapo 2028.

Afrika Kusini imeendelea kutumia utalii kama nyenzo ya kukuza uchumi kupitia maboresho ya sera za usafiri, ikiwamo mfumo wa idhini ya usafiri wa kielektroniki (eTA) huku Kenya ikiendelea kuimarisha nafasi yake Afrika Mashariki kupitia kampeni za kimataifa za kuitangaza nchi hiyo pamoja na kurahisisha taratibu za kuingia kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika. Tunisia imeendelea kuimarisha sekta ya utalii kwa kuboresha huduma, kuongeza uwekezaji katika maeneo ya fukwe na urithi wa kihistoria, hatua iliyoifanya kuvuka watalii milioni 11 mwaka 2025.

Pamoja na ushindani huo, Tanzania inaendelea kujijengea nafasi yake kupitia sera zinazolenga kuongeza ubora wa huduma, kuendeleza utalii wa asili, utalii wa fukwe, utalii wa mikutano na utalii wa kitamaduni. Kampeni za kimataifa kama The Royal Tour na Amazing Tanzania zimechangia kuongeza utambulisho wa vivutio vya Tanzania katika masoko mbalimbali duniani.

Hata hivyo sekta ya utalii duniani inaendelea kuimarika baada ya athari za janga la Covid-19. Takribani watalii milioni 307 walisafiri kimataifa katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 ikiwa ni ongezeko la karibu milioni sita ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025. Mwaka 2025 dunia ilirekodi zaidi ya watalii bilioni 1.5, hali inayoonesha kurejea kwa kasi kwa sekta hiyo.

Kwa Tanzania, mwenendo huo wa dunia unatoa fursa ya kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na sekta hiyo. Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa mafanikio ya kufikia lengo la watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030 yatategemea kuendelea kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha usafiri wa anga, kuongeza uwekezaji katika huduma za malazi na kuendeleza masoko mapya ya utalii ili kuifanya Tanzania izidi kuwa miongoni mwa vinara wa utalii barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *