
Dar es Salaam. Wakazi wa Mitaa ya Pingoni na Thaluji jijini Tanga, wamedai kuwa wapo hatarini kupata changamoto za kiafya, zinazotokana na uvutaji wa moshi na vumbi linalotoka katika kiwanda cha kuzalisha chokaa na gypsum.
Wakizungumza hivi karibuni wananchi hao wamedai kuwa licha, ya mamlaka za Serikali kukifungia kiwanda hicho kwa kukiuka taratibu ikiwamo sheria za mazingira, hali bado kutokana na uzalishaji kuendelea.
Hata hivyo, uongozi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Kampuni ya Nanfang, umesema hakuna shughuli zozote zinazoendelea kwa sababu zilisitishwa na Serikali tangu Septemba mwaka 2025 ili kupisha maboresho ya kukabiliana na changamoto hizo.
Wakazi wamedai moshi, vumbi na harufu kali inayotoka kiwandani hapo imeendelea kuwasababishia changamoto za kiafya, huku wakisisitiza kuwa hawapingi uwekezaji bali wanataka mazingira salama yatakayolinda afya za wananchi wanaoishi jirani.
Kwa mujibu wa makamu mwenyekiti wa wakazi wa Pingoni, Ismail Banda, wananchi waliwasilisha kilio chao hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian aliyewahi kufika kiwandani hapo akiambatana na wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kuunga mkono maelekezo ya kutaka kifungwe.
Katika ziara hiyo, Dk Batilda alibaini upungufu katika kiwanda hicho ikiwamo ya kutokuwa na mifumo ya uokozi, hivyo aliungana na NEMC kutaka kisitishwe shughuli zake ili kupisha maboresho.
Mbali na hilo, Dk Batilda aliwaomba wawekezaji hao kutumia teknolojia ya kisasa katika kukabiliana changamoto ya vumbi na moshi unaokwenda kwa wananchi.
Pia, aliagiza kifanye tathimini ya athari ya mazingira.
“Hata hivyo, Baada ya muda shughuli za uzalishaji zilianza tena na hali ikawa mbaya zaidi, hatupingi uwekezaji wala kiwanda kifungwe. Tunachokitaka marekebisho yafanyike ili kisihatarishe afya za wananchi,” alisema Banda.
Uongozi wajibu
Akizungumza na Mwananchi, mwakilishi wa kiwanda hicho, Given Mangula amedai tangu mwaka jana kiwanda kilisimamishwa na Dk Batilda pamoja na maofisa wa NEMC kwa masharti ya kuhakikisha moshi na vumbi haliendi kwa wananchi.
“Baada ya hapo tulisimama na kuanza kusimika teknolojia ya mitambo itakayozuia moshi na vumbi visiende kwa wananchi chini ya usimamizi mkali wa NEMC,”
“Hadi sasa tunavyoongea kiwanda kimesimama hakitoi huduma zozote, kitu kilichofanyika ni majaribio kutokana na mifumo mipya iliyowekwa ya kuzuia moshi na vumbi visiende kwa wananchi,” ameeleza Mangula.
Kwa mujibu wa Mangula, majaribio ya kwanza na pili, yaliyofanyika miezi kadhaa ilionekana bado, lakini ya tatu ilipofanyika ikaonekana kiwanda kimefika kiwango kinachohitajika cha kukabiliana na changamoto hiyo.
“Hadi sasa hatufanyi kazi kwa sababu taratibu fulani za Serikali hazijakamilika, zikikamilika tutakuwa sehemu sahihi ya kuanza uzalishaji,” amesema.
“Hayo malalamiko yangekuwa mwaka jana ingekuwa sawa, lakini mwaka huu kiwanda kimesimama kwa muda mrefu sana,” amesisitiza Mangula.
Katika maelezo yake, mkazi Pingoni na mjumbe wa Serikali ya Mtaa, Mono Kitone, amesema amewahi kufanya kazi katika kiwanda hicho kwa mwezi mmoja, hata hivyo alilazimika kuacha kutokana na mazingira aliyoyataja kuwa hatarishi kwa afya.
Kitone amedai harufu kali, joto na ubora hafifu wa vifaa vya kujikinga vilimsambabishia matatizo ya kifua na ngozi, hali iliyomfanya kuacha kazi kiwandani hapo.
Mbali na huyo, mwananchi mwingine wa Pingoni, Mamyaki Msharo, amemshukuru Rais Samia na Dk Batilda kwa hatua walizowahi kuchukua, lakini bado kiwanda kinaendelea na uzalishaji.
“Watoto wadogo wamekuwa wakipata matatizo ya kifua na kulazwa mara kwa mara kwenye vituo vya afya,” amedai.
Kwa upande wake, Haidi Hizza amesema moshi unaotoka usiku pamoja na harufu kali umekuwa ukiwasababishia kikohozi na matatizo ya mfumo wa upumuaji.
“Naogopa hata kwenda kuomba ajira kiwandani kutokana na hofu ya usalama wa mazingira ya kazi,” ameeleza.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Thaluji, Andrea Mhile, amethibitisha kupokea malalamiko ya wananchi na kuyafikisha katika ngazi za wilaya na mkoa, hatua iliyomfanya Dk Batilda kufika eneo hilo mara mbili na kutoa maelekezo.
“Tunawapenda wawekezaji kwa sababu wanatoa ajira na kuchochea uchumi. Tunaiomba Serikali ifuatilie kwa kina suala hili ili wananchi wanufaike na matunda ya maendeleo katika mazingira salama,” amesema Mhile.