Moshi. Waziri wa Afya ambaye pia ni mlezi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mohammed Mchengerwa amewataka viongozi na watendaji wa Serikali mkoani humo kuwa karibu na wananchi kwa kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili badala ya kusubiri viongozi wa ngazi za juu kufika katika maeneo yao.

Amesema viongozi wengi wana mamlaka ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hivyo hawapaswi kusubiri Mkuu wa Mkoa, mawaziri au viongozi wa kitaifa ndipo wachukue hatua.

Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Julai 25, 2026 wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro na wananchi wa Manispaa ya Moshi baada ya kukagua uwanja wa michezo uliopo Kata ya Majengo.

“Viongozi piteni nyumba kwa nyumba kupokea kero za wananchi. Msijifungie ofisini, tokeni mkawasikilize wananchi katika maeneo yao,” amesema.

Amesema dhamana waliyopewa viongozi ni ya kuwatumikia wananchi, hivyo wanapaswa kujishusha na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwajibikaji.

“Kama kuna changamoto mnazoweza kuzitatua, zimalizeni. Msisubiri Mkuu wa Mkoa, Waziri au viongozi wa kitaifa waje. Zile zilizo ndani ya mamlaka yenu zipatieni ufumbuzi,” amesema.

Aidha, amewataka wenyeviti wa vijiji na mitaa kusimamia kikamilifu maeneo yao kwa kuzingatia taratibu za uongozi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili.

Mchengerwa amesema uzembe wa baadhi ya viongozi na watendaji ni miongoni mwa vikwazo vinavyochelewesha maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Adui mkubwa wa maendeleo ni sisi wenyewe. Kama kila mmoja atatekeleza wajibu wake kwa wakati, changamoto nyingi zinazowakabili wananchi zitamalizika,” amesema.

Amekumbusha kuwa madaraka ni ya muda, hivyo viongozi hawapaswi kuyaona kama nafasi ya kujisitiri badala ya kuwahudumia wananchi.

“Madaraka ni koti; leo unalo, kesho unaweza usiwe nalo. Tusione vyeo ni sehemu ya kwenda kupumzika. Lazima tufanye kazi kwa bidii, kwa sababu huo ndiyo mtaji wetu,” amesema.

Waziri huyo pia amewahimiza wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kulinda amani ya nchi, akisema maendeleo ya Taifa yanategemea uwajibikaji wa viongozi na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewataka watumishi wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima inayoweza kudhoofisha utoaji wa huduma.

“Tufanye kazi, hayo ndiyo maelekezo yangu. Lakini mambo binafsi tusiumizane. Mkoa wetu umetulia, hivyo kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa maslahi ya wananchi,” amesema Babu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *