Dar es Salaam. Wakati Rais wa Botswana, Duma Boko, akiwahimiza watu kutobakia kwenye uhusiano wenye sumu, uliovunjika au usio na furaha kwa ajili tu ya kulinda heshima ya ndoa, ujumbe huo unaonekana kuakisi vyema maisha ya Vivian Shuma.

​Vivian hivi karibuni alitengana kwa amani na mumewe,  baada ya kudumu katika ndoa kwa miaka 15.

​Kauli hiyo ya Rais Boko, aliyoitoa wakati akihutubia  Jeshi la Ulinzi la Botswana (BDF) hivi karibuni, ilizua mjadala mkali na wa kina kote barani Afrika.

Waliomuunga mkono walimsifu kwa kuibua mada ambayo mara nyingi huonekana kama mwiko kuzungumzwa, wakitaja ujumbe wake kuwa ni wa kweli, wenye huruma na uliokuja kwa wakati mwafaka.

​Hata hivyo, wakosoaji walidai kuwa kauli zake ziko hatarini kudhoofisha taasisi ya ndoa,  kwa kuwapa watu ushawishi wa kutengana badala ya kufanya kazi ya kutatua tofauti zao.

​Katika hotuba yake, Boko alisisitiza umuhimu wa afya ya akili, akiwashauri wanandoa kuchagua amani na kutengana kwa wema, badala ya kubaki kwenye ndoa zisizo na afya au kuruhusu migogoro ikue na kugeuka  kuwa ukatili.

​Alifafanua kuwa hakuwa akihamasisha talaka, bali alikuwa akiwahimiza watu kutoa kipaumbele kwa heshima, amani na usalama wa mtu mmoja mmoja.

​Kwa Vivian, ahadi ya ‘mpaka kifo kitutenganishe, ’ hatimaye ilijisalimisha mbele ya ukweli wa maisha. 

Aliondoka katika nyumba yake akihitimisha ndoa ya miaka 15 na kuacha nyuma maisha aliyokuwa ameyajenga pamoja na mumewe na watoto wao wawili. Anasema alifanya uamuzi huo ili kuokoa nafsi yake.

​Muda mfupi baadaye, alifungua shauri la talaka, na kuanza mchakato mrefu wa kisheria uliomchosha sana kihisia na kiroho.

​Malengo yake binafsi, taaluma yake na afya yake ya akili viliathirika vibaya wakati akijaribu kujenga upya maisha ambayo hakuwahi kuyawazia.

Hii ni kwa sababu anasema  aliwekeza miaka mingi ya fedha, hisia na nguvu zake kwa familia ambayo leo imesambaratika.

Uhalisia kwenye jamii

​Kisa cha Vivian si cha kipekee. Kinaakisi maisha ya maelfu ya wanaume na wanawake wanaokabiliana na athari za kihisia, kisaikolojia na kifedha zinazotokana na talaka.

Ni hali inayoibua swali la msingi: watu wanawezaje kujijenga upya baada ya kutengana?

​“Nilichukua uamuzi sahihi wa kuondoka. Hata hivyo, ulikuja na msisimko na kuvurugika pakubwa kwa maisha. Uliathiri ustawi wangu, taaluma yangu, maisha ya watoto wangu shuleni na nyumbani, na pia ulimwathiri mume wangu wa zamani kisaikolojia, kimwili na kifedha, ” anasema Vivian.

​Anaongeza: “Talaka ni miongoni mwa uzoefu mgumu zaidi ambao mtu anaweza kupitia, hasa wakati familia inapokuwa haijajiandaa. Kama mshtuko huo hautadhibitiwa vyema, unaweza kuathiri familia kwa upana zaidi.”

​Mwanasikolojia, Cosmas Madulu, anasema mara nyingi talaka huanzisha mchakato wa kuomboleza unaofanana kabisa na msiba wa kifo.

​“Watu hupitia hatua za kukataa ukweli, hasira, huzuni na hatimaye kukubali matokeo. Mchakato huu hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine, na hakuna muda maalum uliowekwa wa kupona,” anasema.

​Anaongeza kuwa watu wengi hukandamiza hisia zao, kwa sababu jamii inatarajia wasonge mbele kwa haraka.

​“Uponyaji huanza pale watu wanapokubali maumivu yao badala ya kujifanya kuwa kila kitu kiko sawa. Majeraha ya kihisia yakipuuzwa, yanaweza kukua na kuwa msongo wa mawazo na wasiwasi uliopitiliza,” anaeleza.

​Naye  mkufunzi na mfanyabiashara, Charles Nduku, anasema mara nyingi talaka humwacha mtu akiwa amebeba majukumu yaliyokuwa yakigawanywa hapo awali.

​“Watu waliotengana hivi karibuni wanaweza kujikuta wakitakiwa kutengeneza bajeti mpya, kutafuta vyanzo vya ziada vya mapato au kujenga upya akiba zao baada ya kugawana mali,” anasema. 

Anawasihi watu  kutochukua uamuzi mkubwa wa kifedha, wanapokuwa kwenye msongo wa kihisia.

​“Kuuza mali kwa haraka, kuchukua mikopo isiyo ya lazima au kufanya uwekezaji wa kukurupuka chini ya shinikizo la kihisia,  kunaweza kutengeneza matatizo makubwa zaidi ya kifedha. Hatua ya kwanza inapaswa kuwa kuandaa mpango halisi wa kifedha,” anasema.

​Pia anashauri kupitia upya sera za bima, wosia, walioteuliwa kunufaika na wosia na mipango ya uwekezaji, ili kuakisi mazingira mapya ya kibinafsi.

​Kwa wanandoa wenye watoto, kipaumbele kinapaswa kuhama kutoka kwenye migogoro na kwenda kwenye ushirikiano, anasema Edwick Mapalala, Mkurugenzi wa Shirika la Regional Psychosocial Support Initiative (REPSSI) nchini.

​Anasema watoto mara nyingi huteseka kimya kimya wakati wa talaka na hawapaswi kabisa kutumiwa kama wajumbe au kuingizwa kwenye migogoro ya wazazi.

​“Watoto wanahitaji kuhakikishiwa kuwa wazazi wote wawili bado wanawapenda. Kudumisha ratiba zinazoeleweka, mawasiliano ya wazi na ushirikiano wa kuwalea kwa heshima kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa maumivu ya kihisia. Ndoa inaweza kuisha, lakini uzazi unaendelea,” anasema.

​Mchungaji wa Kanisa la Kipentekoste, Humphrey Shobeza, anasema talaka inaweza kuashiria mwisho wa sura moja ya maisha lakini haipaswi kufafanua hatima ya mtu.

​“Pamoja na maombi, kusamehe na kukubali kuwa maisha yanabadilika, watu wanaweza kugundua tena mwelekeo mpya na kuanza upya,” anasema.

​Mjadala uliorejeshwa na kauli za Rais  Boko uliibuka tena baada ya kuhoji kwanini kiwango kinachoongezeka cha talaka kinaonekana kwa mtazamo hasi pekee.

 Alidai kuwa kutengana kwa amani wakati mwingine kunaweza kuwa bora kuliko kubaki kwenye ndoa zenye ukatili au zisizokuwa na afya.

​Kauli zake zilivuta sifa na ukosoaji kwa pamoja. Hata hivyo, wasiwasi kuhusu kubadilika kwa mifumo ya ndoa unavuka mipaka ya Botswana.

​Utafiti wa mwaka 2026 uliochapishwa kwenye jarida la International Journal of Sociology, ulibaini kuwa viwango vya juu vya utandawazi wa kijamii na kiuchumi vilihusishwa na kuongezeka kwa viwango vya talaka katika nchi 120. Utafiti huo ulihitimisha kuwa uhusiano huo ulikuwa imara zaidi katika jamii ambazo uhuru wa mtu binafsi na usawa wa kijinsia vimepanuka.

​Kesi zinazoongezeka

​Takwimu rasmi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum zinaonyesha kuongezeka kwa migogoro ya ndoa nchini Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.

​Akiwasilisha bajeti bungeni mapema Juni, 2026, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima alisema jumla ya migogoro 49,573 inayohusu ndoa iliripotiwa kwenye mfumo wa ustawi wa jamii kati ya Julai 2025 na Aprili 2026.

​Kati ya hiyo, mashauri 9,995 yalifungwa, 8,036 yalielekezwa mahakamani, huku 31,542 yakibaki chini ya usuluhishi hadi kufikia Juni, 2026.

 Takwimu hizo zinaonyesha ongezeko ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo kesi 31,380 zilirekodiwa mwaka 2024/25 na kesi 28,773 mwaka 2022/23.

​Wachambuzi wanahusisha ongezeko hilo na mambo kadhaa, ikiwemo kuongezeka kwa shinikizo la kiuchumi, kubadilika kwa mifumo ya kifamilia na maandalizi duni kabla ya kuingia kwenye ndoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *