
Magonjwa hayo ni pamoja na kipandauso, kiharusi, kifafa, ugonjwa wa kusahau aia ya Alzheimer, matatizo mengine ya kupoteza kumbukumbu na usonji.
Takwimu hizo ni sehemu ya utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la The Lancet na kuongozwa na watafiti kutoka Shirika la Afya la Nchi za Amerika, PAHO.
Watu milioni 1.1 walifariki mwaka 2023
Magonjwa ya mfumo wa neva huathiri ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu. Yanaweza kudhoofisha uwezo wa mtu kutembea, kukumbuka, kujifunza, kuwasiliana na kudhibiti tabia.
Mwaka 2023, magonjwa hayo yalisababisha takribani vifo milioni 1.1 na miaka milioni 37.5 ya maisha yenye afya kupotea kutokana na vifo vya mapema, magonjwa au ulemavu.
Kipandauso kilitajwa kuwa chanzo kikuu cha miaka ya maisha yenye afya iliyopotea, kikifuatiwa na ugonjwa wa Alzheimer na aina nyingine za kupoteza kumbukumbu, kiharusi kinachotokana na kuziba kwa mishipa ya damu na kuvuja damu ndani ya ubongo.
Kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, kasoro za mirija ya neva, usonji na kifafa zilikuwa miongoni mwa sababu kuu za matatizo hayo.
Kipandauso kiliongoza miongoni mwa vijana, huku Alzheimer, magonjwa mengine ya kupoteza kumbukumbu na kiharusi yakiwaathiri zaidi wazee.
Magonjwa mengi yanaweza kuzuilika
Utafiti umebaini kuwa sehemu kubwa ya madhara ya magonjwa ya mfumo wa neva inaweza kuzuilika kupitia mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Shinikizo la juu la damu lilitajwa kuwa sababu kuu ya hatari ya kupata kiharusi, huku kiwango cha juu cha sukari kwenye damu kikichangia kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa Alzheimer na aina nyingine za kupoteza kumbukumbu. Uchafuzi wa hewa na kuathiriwa na madini ya risasi pia vilitajwa kuwa vihatarishi muhimu.
PAHO yataka mifumo ya afya ibadilike
Mtaalamu wa takwimu za afya kutoka PAHO na mwandishi mkuu wa utafiti huo, Ramón Martínez, amesema watu wengi zaidi sasa wanafanikiwa kuishi baada ya kupata magonjwa ya mfumo wa neva, lakini wanaendelea kuishi kwa muda mrefu na athari zake.
Kutokana na hali hiyo, PAHO imesema mifumo ya afya inapaswa kuimarisha kinga, huduma za ukarabati, matunzo ya muda mrefu na huduma za kuwasaidia watu wenye ulemavu.
Ingawa viwango vya vifo vilipungua kati ya mwaka 1990 na 2023, idadi ya watu walioathirika iliendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu na kuzeeka kwa jamii. Utafiti huo ulichunguza magonjwa 19 ya mfumo wa neva katika nchi na maeneo 38 ya Amerika.