Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani hatua mpya za Marekani na Israel zinazolenga Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), likitaka kuchukuliwe hatua za dharura za kimataifa dhidi ya kampeni ya “Wazayuni-Marekani” ya kutaka kulisambaratisha shirika hilo.

Harakati hiyo imetoa taarifa ikipinga muswada unaoungwa mkono na vyama viwili vikuu vya Marekani uliowasilishwa katika Bunge la nchi hiyo unaotaka kuvunja UNRWA na kuanzishwa kile kinachoitwa “bodi mbadala ya masuala ya kibinadamu.”

Hamas imelitaja pendekezo hilo kuwa ni hatua nyingine kuelekea upande wa kufuta mamlaka ya kihistoria ya shirika hilo na majukumu ya kimataifa.

Hamas imesema muswada huo unalenga kukomesha kazi za UNRWA licha ya mamlaka yake ya kisheria ya kuwahudumia mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu na katika nchi jirani.

Harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina imesisitiza kwamba kubadilishwa shirika hilo hakutafuta suala la wakimbizi wa Palestina wala kubatilisha haki za wakimbizi zinazotambuliwa kimataifa.

Zaidi ya hayo, afisa mwandamizi wa Hamas, Ali Baraka amelaani kampeni ya Marekani na Israel dhidi ya shirika la Umoja wa Mataifa la UNRWA, akiitaja kuwa ni “ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa” na “shambulio la moja kwa moja dhidi ya haki ya kurudi nyumbani kwa wakimbizi wa Kipalestina waliofukuzwa katika nchi yao mwaka wa 1948.”

“UNRWA, iliyoanzishwa chini ya Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa nambari 302 la 1949, si shirika la kutoa misaada tu bali ni shahidi wa kimataifa wa Nakba ya Palestina,” amesema Baraka.

Ameongeza kuwa shirika hilo linaakisi majukumu ya kisheria, kisiasa na kimaadili ya jamii ya kimataifa kwa wakimbizi wa Palestina hadi litakapotimizwa Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa nambari 194, ambalo linadhamini haki yao ya kurudi nyumbani na kulipwa fidia.

Afisa huyo wa Hamas ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, nchi wafadhili na jamii pana ya kimataifa kupinga mashinikizo ya Marekani na Israel, kuhakikisha ufadhili endelevu kwa UNRWA, na kuimarisha elimu, huduma za afya, misaada na huduma za kijamii za shirika hilo huko Gaza, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, Lebanon, Syria, na Jordan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *