
Mkuu wa Jeshi la Uganda na mwana wa Rais aliyechaguliwa tena, Yoweri Museveni, amesema leo Ijumaa kwamba wafuasi 30 wa upinzani wameuawa na 2,000 wamekamatwa kufuatia uchaguzi wa karibuni nchini humo.
Kiongozi wa upinzani, Bobi Wine, amendelea kuwa mafichoni leo Ijumaa baada ya kuwatuhumu askari usalama kuwa walivamia nyumba yake baada ya uchaguzi wa Januari 15. Bobi Wine ameutaja uchaguzi huo kuwa ni “wizi wa aibu” na kuwahimiza watu kuandamana.
“Tumewakamata zaidi ya majambazi 2,000 ambao Kabobi alidhani kwamba angeweza kuwatumia,” ameandika Mkuu wa Jeshi la Uganda, Muhoozi Kainerugaba kwenye mtandao wa kijamii wa X, akitumia jina lake la utani la Wine. Muhoozi ameongeza kuwa: “Hadi sasa, tumewaua magaidi 30 wa NUP,” akimaanisha chama cha Bobi Wine, Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (National Unity Platform).
Kainerugaba, mwenye umri wa miaka 51, anajulikana kwa machapisho yake ya uchochezi kwenye mitandao ya kijamii. Ameeleza waziwazi nia yake ya kumrithi baba yake, na wiki hii ametishia kumsaka na kumuua Robert Kyangulani maarufu kama Bobi Wine.
Miongoni mwa waliokamatwa katika siku za hivi karibuni nchini Uganda ni mbunge wa upinzani, Muwanga Kivumbi, kutoka eneo la Butambala katikati mwa Uganda, ambapo kuliripotiwa ghasia mbaya zaidi za siku ya uchaguzi.
Kivumbi aliiambia AFP kwamba askari usalama waliwaua maafisa wake kumi wa kampeni baada ya kuvamia nyumba yake, huku polisi wakisema wafuasi wake walipigwa risasi baada ya kujaribu kuchoma moto kituo cha kuhesabia kura na kituo cha polisi.
Wakili wa kambi ya upinzani nchini Uganda ameambia AFP kwamba zaidi ya watu 600 wamekamatwa katika maandamano ya baada ya uchaguzi.
Museveni, mwenye umri wa miaka 81, alishinda muhula wa saba wa urais kwa kupata asilimia 72 ya kura, akifuatiwa na Bobi Wine aliyepata asilimia 25 ya kura. Waangalizi wa Afrika na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa walikosoa ukandamizaji mkubwa wa upinzani na kufungwa kwa intaneti.