
“Watu wanafuatiliwa na kukamatwa, wakati mwingine kwa nguvu, ikiwemo katika hospitali, makanisa, misikiti, mahakama, masoko, shule, na hata ndani ya nyumba zao wenyewe, mara nyingi kwa tuhuma tu za kuwa wahamiaji wasio na nyaraka. Watoto wanakosa kwenda shule na miadi ya madaktari wa watoto kwa hofu ya kutowaona wazazi wao tena,” amesema Türk.
“Wale wanaothubutu kuzungumza au kuandamana kwa amani kupinga misako mikali ya uhamiaji wanadhalilishwa na kutishwa na maafisa, na wakati mwingine wenyewe hukumbwa na vurugu za kiholela.”
“Ninashangazwa na unyanyasaji na udhalilishaji wa wahamiaji na wakimbizi ambao sasa umekuwa wa kawaida,” amesema Türk.
Ameohoji akisema, “kujali utu wao na ubinadamu wetu wa pamoja uko wapi?”
Bwana Türk amesema kuwa sera nyingi za uhamiaji zinazotekelezwa sasa na mamlaka za Marekani zinasababisha kukamatwa na kuwekwa kizuizini kiholela na kinyume cha sheria, pamoja na maamuzi yenye dosari ya kuwafukuza watu nchini. Ameeleza wasiwasi kwamba utekelezaji wa sera hizi mara nyingi hauzingatii tathmini za mtu mmoja mmoja kwa kiwango cha kutosha.
“Serikali zina mamlaka ya kuanzisha sera zao za kitaifa za uhamiaji, lakini hili lazima lifanyike kwa kuzingatia kikamilifu sheria. Kuheshimu taratibu za kisheria ni muhimu kwa uhalali na uaminifu wa sera yoyote. Kanuni hizi zisipofuatwa, kwa upana zaidi zitaathiri imani ya umma, kupunguza uhakika wa kisheria, kudhoofisha uhalali wa taasisi, na kukiuka haki za watu binafsi,” amesema Türk.
Watetezi
Aidha ametambua juhudi za maafisa wengi wa umma, makundi ya kijamii na wawakilishi wa asasi za kiraia kote Marekani , Wabunge, majaji, viongozi wa majimbo na serikali za mitaa, pamoja na wanasheria, viongozi wa dini, watoa huduma, wanaharakati, na raia wa kawaida, miongoni mwa wengine wengi wanaosimama kutetea utu, haki na uwajibikaji katika namna wahamiaji na jamii zao wanavyotendewa.
Ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu simulizi zinazodhuru na kudhalilisha utu zinazotumiwa mara kwa mara kuelezea wahamiaji na wakimbizi.
“Historia ya Marekani imeundwa kwa kiasi kikubwa na mchango ambao wahamiaji, kutoka pande zote za dunia, wametoa na wanaendelea kutoa. Kuwatambua wahamiaji na wakimbizi wote kwa pamoja kama wahalifu, vitisho, au mzigo kwa jamii kwa misingi ya asili yao, utaifa au hali yao ya uhamiaji ni kinyume cha utu wa binadamu, si sahihi, na kunapingana na misingi na nguzo za taifa lenyewe,” amesema Türk.
“Natoa wito kwa viongozi katika ngazi zote nchini Marekani kusitisha matumizi ya mbinu za kulaumu wengine kama njia ya kupotosha na kugawa, ambazo huongeza hatari kwa wahamiaji na wakimbizi kukumbwa na uhasama wa chuki dhidi ya wageni na unyanyasaji.”
Türk amelaani matumizi ya oparesheni kubwa za utekelezaji wa sheria na mawakala wa uhamiaji wa Marekani na wengine, ambao mara kwa mara wametumia nguvu zinazoonekana kuwa zisizo za lazima au kupita kiasi.
“Chini ya sheria za kimataifa, matumizi ya nguvu ya kuua kwa makusudi yanaruhusiwa tu kama hatua ya mwisho kabisa dhidi ya mtu anayewakilisha tishio la karibu kwa maisha,” amesema Türk.
Watu wanaokamatwa na kuwekwa kizuizini mara nyingi hukosa kupata kwa wakati msaada wa kisheria na njia madhubuti za kupinga kizuizi chao, pamoja na maamuzi ya kuwafukuza nchini.
Kutenganisha familia
Türk amebainisha kuwa kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kufukuzwa nchini mara nyingi hufanyika bila juhudi za kutathmini na kulinda umoja wa familia, hali inayowaweka watoto hasa katika hatari ya madhara makubwa na ya muda mrefu. Visa vya mara kwa mara vya wazazi waliokamatwa kuhamishwa kati ya vituo vya kizuizini, bila kupewa taarifa za kutosha kuhusu walipo au upatikanaji wa msaada wa kisheria, pia vinazuia uwezo wao wa kuwasiliana na familia zao na wawakilishi wao wa kisheria.
“Natoa wito kwa Serikali kusitisha vitendo vinavyosambaratisha familia,” amesema Kamishna Mkuu.
Vifo
Pia ametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru na wa uwazi kuhusu ongezeko linalotia wasiwasi la idadi ya vifo chini ya ulinzi wa Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE). Takribani vifo 30 viliripotiwa mwaka jana 2025, na vingine sita vimeripotiwa hadi sasa mwaka huu.
Nchi zisizo zao
Türk ameeleza kuwa baadhi ya uhamisho wa watu kwenda nchi nyingine, ikiwemo zile zisizo nchi zao za asili au ambazo hawana uhusiano nazo, umefanywa kwa haraka bila kuzingatia ipasavyo hatari ya mateso au madhara yasiyorekebishika. Pia kumekuwepo na makosa yaliyokubaliwa na mamlaka, ambapo watu wamefukuzwa kimakosa kutoka Marekani. Kesi hizi zinaonesha hitaji la kuwepo kwa ulinzi imara zaidi, ameongeza.
“Marekani ina wajibu wa kuzingatia sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za wakimbizi. Utekelezaji wa uhamiaji lazima kila wakati uheshimu taratibu za kisheria, ulinzi dhidi ya kizuizini kiholela, kanuni ya kutorejesha watu mahali wanapokabiliwa na hatari usawa na kutobagua, pamoja na ulinzi wa familia,” amesisitiza Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa.