Muswada wa fedha 2026 nchini Kenya unatarajiwa kutiwa saini na kuwa sheria.

Rais William Ruto wa Kenya kesho Jumanne anatarajiwa kutia saini kuwa sheria muswada wenye utata wa Fedha wa mwaka 2026, hatua itakayofungua njia ya utekelezaji wa sheria itakayowezesha ufadhili wa bajeti ya taifa ya shilingi trilioni 4.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mswada huo umeibua mjadala mkali nchini Kenya, huku wadau mbalimbali wakieleza maoni tofauti kuhusu athari zake kwa uchumi na maisha ya wananchi.

Akizungumza katika Ikulu ya Rais siku ya Jumapili jijini Nairobi, Rais William Ruto alisema kupitia mswada huo, serikali yake imeweka mikakati ya kutimiza ahadi za maendeleo walizotoa kwa wananchi.

Hata hivyo upinzani unasema ikiwa mswada huo utatiwa saini kama ulivyo, huenda ukasababisha kupanda zaidi kwa gharama za maisha nchini Kenya.

Gavana wa Siaya James Orengo anasema mswada huo ulipitishwa bila ushiriki wa maana kutoka kwa Wabunge wengi.

Wabunge 122 walipiga kura ya kuunga mkono, 40 wakapiga kura ya kupinga, huku 187 wakikosa kushiriki.

Haya yanajiri wakati vijana wa Gen Z wakipanga kufanya maandamano ya kumbukizi ya wenzao waliofariki miaka miwili iliyopita wakati wa maandamano ya kupinga mswada sawia na huo wa Fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *