RUVUMA: Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeanza rasmi maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Peramiho, lililokuwa likiongozwa na aliyekuwa Mbunge, Jenista Mhagama, huku ikisisitiza kuwa uzingatiaji wa sheria, taratibu na ushirikishwaji wa wadau wote wa uchaguzi ndiyo njia pekee ya kupunguza au kuondoa kabisa malalamiko na vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Hatua hiyo imeanza kwa kuwajengea uwezo watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa, jimbo na kata ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, utulivu na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi yanayofanyika mjini Iringa kuanzia Januari 24 hadi 26, 2026, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, alisema kuwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Peramiho pamoja na uchaguzi wa udiwani katika Kata ya Shiwinga unafanyika kufuatia nafasi hizo kuwa wazi kwa mujibu wa sheria, hali iliyolazimu Tume kuanza mchakato wa maandalizi mapema ili kulinda uhalali na uaminifu wa uchaguzi huo.

Jaji Mwambegele alisema kuwa mafunzo hayo yanawahusisha waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata, maafisa uchaguzi, maafisa ununuzi na wahasibu, ambao wote wana jukumu la moja kwa moja katika kusimamia na kuratibu mchakato mzima wa uchaguzi.
Alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha majukumu yao ya kisheria, kuwajengea uelewa wa kina kuhusu taratibu za uchaguzi na kuwaandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Tume, uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua nyingi za kisheria ambazo zinapaswa kuzingatiwa kwa umakini mkubwa, kuanzia maandalizi ya awali, uteuzi wa watendaji, maandalizi ya vituo vya kupigia kura hadi siku ya kupiga kura na hatua za baada ya uchaguzi.

Alisisitiza kuwa kufuata taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa huru, wa haki na wenye ufanisi, hali itakayopunguza au kuondoa kabisa malalamiko na vurugu zinazoweza kujitokeza.
Aliwaonya watendaji wa uchaguzi dhidi ya kufanya kazi kwa mazoea, akisema kuwa kila uchaguzi una mazingira na changamoto zake.
Alisisitiza kuwa maelekezo yanayotolewa na Tume yanapaswa kuzingatiwa kikamilifu bila upendeleo, huku akiwataka watendaji wote kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwazi.
Aidha, Jaji Mwambegele alisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha kwa karibu vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili pamoja na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo husika.

Alisema kuwa ushirikishwaji huo ni nyenzo muhimu ya kujenga uaminifu, kuondoa mashaka yasiyo ya lazima na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya watendaji wa uchaguzi katika Jimbo la Peramiho na Kata ya Shiwinga.
Katika kuelekea uchaguzi huo, aliwataka waratibu na wasimamizi wa uchaguzi kufanya utambuzi wa mapema wa vituo vya kupigia kura na miundombinu ya kufika katika vituo hivyo, ili kubaini mahitaji maalum na kuweka mpangilio mzuri utakaowezesha uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
Pia aliwakumbusha kuhakikisha wanaajiri watendaji wa vituo wenye weledi na sifa stahiki, badala ya kuzingatia upendeleo wa kindugu au kijamii, jambo ambalo linaweza kuathiri uaminifu wa mchakato mzima wa uchaguzi.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuhakiki vifaa vya uchaguzi vinavyopokelewa kutoka Tume na kuhakikisha vinasambazwa kwa wakati katika vituo vyote, pamoja na kuweka utaratibu utakaowezesha vituo vya kupigia kura kufunguliwa kwa wakati uliopangwa siku ya uchaguzi.
Akizungumzia matarajio ya Tume, Jaji Mwambegele alisema kuwa baada ya mafunzo hayo ya siku tatu, watendaji wote wa uchaguzi wanatarajiwa kuwa na elimu na ujuzi wa kutosha wa kusimamia na kuratibu uchaguzi huo mdogo.
Naye Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Ruvuma, Athumani Kateula, amewahimiza wananchi wenye sifa katika Jimbo la Peramiho kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi ya ubunge, kushiriki kikamilifu katika kampeni na hatimaye kujitokeza siku ya uchaguzi kuchagua kiongozi mwenye sifa.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbozi, Danny Tweve, amesema maandalizi ya Uchaguzi wa Diwani Kata ya Shiwinga yanaendelea vizuri, akibainisha kuwa wamejipanga kuhakikisha hatua zote za uchaguzi kuanzia uteuzi wa wagombea, kampeni hadi siku ya kupiga kura zinasimamiwa kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.
Kabla ya kufunguliwa rasmi kwa mafunzo hayo, wasimamizi wa uchaguzi walikula kiapo cha kujitoa katika uanachama wa vyama vya siasa, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha misingi ya uwazi, haki na kutokuegemea upande wowote katika usimamizi wa chaguzi.