GEITA: WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea hali inayorudisha nyuma kasi ya utekelezaji wa miradi.
Shemdoe ametoa maagizo hayo wakati akizungumza katika kikao cha ndani kilichowakutanisha Watendaji wa idara mbalimbali za Serikali, kilichofanyika katika Manispaa ya Geita.
Shemdoe amesema utendaji wa mazoea hasa ngazi ya halmashauri imekuwa kiini cha miradi mingi kuzorota kutokana na ufuatiliaji hafifu wa miradi inayotekelezwa.
Amesema watendaji wanapaswa kutimiza wajibu wao pasipo kusubiri ziara za Viongozi wa ngazi za juu hali inayopelekea baadhi ya miradi kutekelezwa kinyume cha mkataba.
“Tusisubili kusikia mradi umeharibika ndiyo twende,tuwekw utaratibu wa kutembelea miradi. Tukikuta sehemu nyingine haijatekelezwa vizuri tuchukue hatua”, amesema Profesa Shemdoe.

Aidha Shemdoe amewataka watendaji wa serikali kuzingatia agizo la Waziri Mkuu Januari 23,2026 juu ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili fedha za umma zitumike kwa ufasaha na kuleta matokeo chanya.
Amesema tayari ameshatoa siku 14 kwa wakuu wa Mikoa kuunda kamati za ufuatiliaji wa miradi ili kudhibiti wimbi la miradi ya serikali kusuasua ingali tayari bajeti ilishatengwa kwa ajili ya utekelezaji.
Ameongeza kuwa pia wakuu wa mikoa watapaswa kuwasilisha madokezo yanayoonyesha miradi mipya iliyobuniwa kupitia fedha ambazo matumizi yake yameonekana kutokuwa ya lazima.
Kaimu Mkuu wa mkoa wa Geita ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale Grace Kingalame ameahidi kufanikisha utekelezaji wa maagizo hayo kwa watendaji wote ngazi ya halmashauri na mkoa.
“Tukushukuru Mheshimiwa Waziri,nikuahidi kuwa maagizo yako tumeyapokea na tutayafanyia kazi kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla,” amesema Kingalame.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi, amesema manispaa hiyo itaendelea kusimamia miradi ya Serikali sambamba na kukuza ukusanyaji wa mapato kwa kuzingatia utaratibu.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 Manispaa ya Geita imelenga kukusanya zaidi ya Sh bilioni huku ambapo hadi kufika Januari 2026 halmashauri imefikia asilimia 64 ya lengo hilo.