
Mbeya. Rais Samia Suluhu Hassan, amechangia vifaa vya kidigitali vya kujifunza na kujifunzia wanafunzi wenye mahitaji maalumu shule ya Msingi Nsalala mchanganyiko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi.
Vifaa hivyo ni pamoja na nukta nundu,kompyuta na kifaa maalum cha sauti kwa ajili ya usikivu kwa wanafunzi wenye changamoto ya uziwi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ,Erica Yegella amesema leo Jumatatu Januari 26,2026 ,na kwamba vimetolewa na kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Yegella amesema hayo wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa shule ambavyo vitasaidia kuongeza ufanisi wa namna ya bora ya kujifunza na kujifunzia wanafunzi na walimu katika kutekeleza sera ya elimu kuelekea matumizi mitaala mipya nchini.
“Leo Januari 26, 2026 mwaka huu tumekabidhi vifaa kwa uongozi wa shule ya msingi Nsalala mchanganyiko hususani nukta nundu boksi tano,kompyuta na kifaa maalumu cha sauti kitakacho saidia usikivu kwa wanafunzi ambavyo vimetolewana Rais Samia Suluhu Hassan, “amesema.
Amesema kutokana na hatua hiyo wana kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa namna inavyo tatua changamoto katika sekta ya elimu maalumu jambo ambalo litaongeza hamasa kwa wanafunzi kusoma kwa bidiii kama jamii nyingine na kuacha kukaa majumbani.
Katika hatua nyingine, Yegella amewataka walimu kuvitunza na kutumia kama nyenzo pekee ya kuongeza ufauru kwa wanafunzi hao hususani wanaotumia kifaa cha nukta nundu na sauti.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Divisheni ya Awali na Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ,Tanu Kameka amesema wana kila sababu kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuchangia vifaa hivyo vya kidigitali jambo ambali litaongeza ufanisi wa kupata elimu bora na kuongeza ufauru.
“Mengi tunaona Rais ameyafanya katika kuboresha miundombinu ya elimu,lakini kubwa zaidi ametupia jicho wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambao watu wanaweza kudhani hawawezi kufanya kitu katika jamii ,”amesema.
Amesema vifaa hivyo vya kidigitali vinakwenda kuleta hamasa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kuongeza weredi katika masomo hususani walimu katika kufundisha mitaala mipya ya kuwajengea ujuzi na maarifa.
Wakati huo huo amesema halmashauri hiyo ina shule 184 kati ya hizo 170 za Serikali, lakini 14 watu binafsi na tano elimu jumuishi ambazo ni Nsalala,Ndola,Mbalizi One,Juhudi na Nsongwi juu.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, John Manase amesema ilianzishwa mwaka 1975 ,kwa kutoa elimu jumuishi ikiwa na wanafunzi 1,194 kati ya hao 49 wenye mahitaji maalumu.
“Tunashukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kuona jambo la msingi la kurejesha tabasamu kwa wanafunzi wa mahitaji maalumu kwa kuboresha miundombinu ya vyumba vya madarasa na mabweni na kuchangia vifaa vya kisasa ,”amesema.
Naye Mwanafunzi mwenye Ulemavu wa Ngozi (Albino) James Kandonga (13),ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuhaidi kusoma kwa bidii ili kuja kuwa tegemezi kwa familia yake na Serikali kwa ujumla.