Unguja. Kesi za waliokuwa wagombea ubunge wa Chama cha ACT-Wazalendo kupinga matokeo katika majimbo 19 ya Unguja zimekwaa kisiki baada ya Mahakama Kuu Zanzibar kukubaliana na pingamizi lililowekwa na mwanasheria mkuu wa Tanzania kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka kusikiliza mashauri yanayotokana na wabunge wa Tanzania.

Hayo yamejiri leo Jumanne, Januari 27, 2025 baada Jaji Haji Suleiman Khamis aliyekuwa akisikiliza mashauri hayo,  kueleza kuwa, Katiba imeifunga mikono Mahakama hiyo katika mashauri ya namna hiyo.

Awali, walipeleka pingamizi kuwa, Mahakama Kuu ya Zanzibar haina uwezo Kikatiba wa kusikiliza mashauri hayo ya uchaguzi na maombi yanayotokana na uchaguzi kwamba inatakiwa kusikilizwa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Akitoa uamuzi mdogo katika pingamizi lililowekwa, Jaji Khamis amesema Mahakama ya Zanzibar inakikomo, hivyo haitakiwi kusikiliza mashauri ya uchaguzi kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano inataka hivyo katika kifungu cha 83 (1) kinachosema mashauri hayo yatasikilizwa kwa Mahakama ya Tanzania.

Pingamizi hilo liliwekwa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu baada ya upande wa madai kuiomba Mahakama kupata punguzo la gharama katika uendeshaji wa kesi hizo.

Mwanasheria wa Serikali, Nalindwa Sekimanga akiwa miongoni mwa jopo la wanasheria kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano, alitaja vifungu mbalimbali vya kisheria, ikiwamo kifungu cha 83 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kinachobainisha kuwa mashauri yote ya uchaguzi yanayohusu wabunge yatasikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Tunaomba Mahakama ikubali pingamizi lililowasilishwa na upande wa Serikali, Mahakama Kuu ya Zanzibar haina uwezo wa kikatiba kusikiliza mashauri yanayohusu mambo ya uchaguzi wa wabunge wa Jamhuri,” amedai Sekimanga.

Kwa upande wao, mawakili wanaowawakilisha waliokuwa wagombea ubunge wa ACT-Wazalendo wakiongozwa na wakili Omar Said Shaaban, wamepinga hoja hiyo wakieleza kuwa, Mahakama Kuu ya Zanzibar ina mamlaka ya kusikiliza mashauri yanayohusiana na Muungano.

Shaaban amenukuu kifungu cha 93 (1) cha Katiba ya Zanzibar na kifungu cha 3(1)(a) cha sheria namba 2 ya 1985 kuwa, ndio kinachoianzisha, na kuipa mamlaka Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Amedai mahakamani hapo kuwa,  mamlaka iliyopewa ni bila ya kikomo (unlimited) kwa mambo yote na sheria zote zinazotumika Zanzibar zikiwamo za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizotungwa na Bunge kama ilivyo Sheria ya Uchaguzi.

“Hivyo, Mamlaka ya Mahakama Kuu Zanzibar hayaondolewi wala hayapimwi na Ibara ya 83 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika ngazi ya Mahakama Kuu,” amedai Wakili Shaaban.

Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili Omar amesema wana namna mbili za kufanya, moja ni kukata rufaa Mahakama ya rufani kuona inaweza kuwa na mtazamo tofauti na njia nyingine ni kwenda Mahakama kuu ya Tanzania.

Kuhusu kuwa nje ya muda, Omar amesema watakwenda kuomba nyongeza ya muda kwasababu walikuja Mahakama ya Zanzibar kwa muda muafaka.

“Tulifungua ndani ya wakati, tulifuata sheria, Mahakama imeona tofauti sasa tutaenda kuomba nyongeza ya muda ili tuweze kufungua kesi katika Mahakama hiyo,” amesema.

Hata hivyo, amesema hayo yatafanyika baada ya kukaa na wateja wao na uamuzi utakotolewa na chama cha ACT Wazalendo.

Naye mmoja wa waliofungua kesi hizo, Yussuf Salim Hussein aliyekuwa mgombea ubunge wa Chambani, amesema hawaridhiki na uamuzi wake kwa kuwa, Zanzibar ni sehemu ya Muungano.

“Sasa kama ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano ipo wapi ofisi ya Mahakama kuu hapa Zanzibar, Mikoa mingine wanafungua kesi kwenye mikoa yao lakini kwanini Zanzibar iende kufungua Mahakama Kuu Dar es Salaam.”

Kesi hizo zilifunguliwa na waliokuwa wagombea ubunge katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 katika majimbo 19 ya Unguja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *