Dar es Salaam. Sweet Fella ambaye ni mke wa meneja wa wasanii, Mkubwa Fella, amesema hali ya afya ya mume wake inaendelea kuimarika, hali inayowapa matumaini makubwa familia na watu wake wa karibu.
Akizungumza na Mwananchi, Sweet Fella anasema kwa sasa mumewe anaendelea vizuri kiafya ikilinganishwa na kipindi cha awali na anaendelea kufanya mazoezi mepesi kwa kuzingatia maelekezo ya madaktari.
Anasema maendeleo yake yanatia moyo mkubwa na yanaonyesha dalili njema za kurejea katika hali yake ya kawaida.
“Hali yake kwa sasa ni nzuri sana ukilinganisha na ilivyokuwa mwanzo kila siku tunashukuru Mungu kwa hatua anayopiga,” anasema Sweet Fella.
Anaongeza, madaktari wamekuwa wakimpa maelekezo maalum ya mazoezi ili kuimarisha mwili wake hatua kwa hatua bila kuathiri afya yake.
“Anafanya mazoezi mepesi kila siku kulingana na ushauri wa madaktari. Hatufanyi mambo kwa pupa, kila kitu kinafanyika taratibu na ana chakula chake maalumu cha kula,” anafafanua.
Anasema familia imekuwa bega kwa bega na mumewe katika kipindi chote cha matibabu, huku sapoti kutoka kwa baadhi ya mashabiki na wadau mbalimbali wa sanaa ikiwapa faraja.
“Upendo na maombi kutoka kwa watu wengi yamekuwa yakimpa nguvu sana. Anajua bado ana nafasi kubwa mioyoni mwa mashabiki wake,” anasema.
Aidha, anafichua Fella mwenyewe ameonyesha ari na dhamira ya kurejea katika shughuli zake mara baada ya afya yake kutengamaa.
“Anajitahidi sana, ana nia ya kuendelea na kazi zake mara tu madaktari watakapomruhusu. Hilo ndilo jambo linalotupa matumaini zaidi.”
“Tunaamini Mungu yupo nasi. Tunaomba watu waendelee kutuombea kwa sababu safari bado ipo, lakini dalili ni nzuri,” anasema.
Anasema licha ya changamoto hiyo, madaktari wameeleza hali hiyo ni sehemu ya mchakato wa kupona na wanaridhika na hatua anazopiga mume wake.
FELLA AZUNGUMZA
Januari 26, 2026, Mwananchi lilizungumza na Fella na hakuwa na uwezo wa kuzungumza maneno mengi, hali iliyodhihirisha wazi anaipambania afya yake na alikuwa akitamka neno moja moja.
“Amina… amina, Asante, Nashukuru.”
Alionekana kutumia nguvu nyingi kujibu na wakati mwingine alikaa kimya kwa muda kabla ya kuitikia kwa ishara au kwa neno fupi, hali iliyoonesha kuwa bado yupo katika hatua ya mwanzo ya kurejea katika uwezo wake wa kuzungumza.
Licha ya hali hiyo, Fella aliendelea kuonyesha utulivu na imani, akitumia neno ‘amina’ kama ishara ya kukubaliana na matumaini ya kuendelea kuimarika kiafya.
KUMTELEKEZA MUMEWE
Aidha Sweet Fella, anakanusha taarifa ya kumtelekeza mumewe kwa kujihusisha na starehe katika maeneo ya baa, hususan baa ya Dizonga iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao hiyo walidai Sweet Fella, amekuwa akijikita zaidi kwenye starehe badala ya kumhudumia mumewe, ambaye kwa kipindi cha hivi karibuni amekuwa akipitia changamoto za kiafya.
Hata hivyo, Sweet Fella aliweka wazi madai hayo hayana ukweli wowote.
“Kinachozungumzwa mitandaoni si kweli kabisa. Ninapofika kwenye maeneo ya starehe, huwa ni kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza miradi na biashara za mume wangu. Nafanya hivyo ili kuhakikisha familia yetu inapata mahitaji ya kila siku, hasa katika kipindi hiki ambacho mume wangu bado anaendelea na matibabu.
“Hiyo baa ya Dizonga inayozungumziwa mimi nashinda hapo ni baa yetu mimi na mume wangu na ni moja ya sehemu ya maisha yangu, huwa nashinda hapo hata kabla hajaanza kuumwa, sasa watu wanataka nimwachie nani asimamie biashara yetu?” anasema Sweet Fella na kuongeza, maisha ya umaarufu yana changamoto nyingi, ikiwemo watu kutoa tafsiri potofu au kutunga taarifa zisizo na ukweli kuhusu maisha binafsi ya watu maarufu,”anasema
Hata hivyo, anasisitiza anaendelea kuwa karibu na mumewe na familia yao kwa jumla, huku akitoa kipaumbele kwa ustawi wa familia kwa kuendelea kujikita katika kuhakikisha miradi ya Fella inaendelea vizuri, huku matumaini yakibaki mumewe ataendelea kuimarika kiafya na kurejea katika shughuli zake za muziki na biashara hapo baadaye.
Fella ni mmoja wa mameneja wa wasanii waliowahi kutoa mchango mkubwa katika tasnia ya muziki nchini na taarifa za kuimarika kwa afya yake zimeendelea kuwapa faraja familia yake na watu wa karibu.