
Marekani. Wakati nguli wa Pop R Kelly akiendelea kutumikia kifungo chake katika gereza la Butner, North Carolina. Huku tayari akiwa amekaa kwa takribani miaka miwili sasa, inaelezwa kuwa muda wake wa kutoka bado sana.
Kwa mujibu wa rekodi za hivi karibuni za Ofisi ya Magereza ya Shirikisho la Marekani (Bureau of Prisons), R. Kelly anatarajiwa kuachiwa huru Desemba 21, 2045. Wakati huo, atakuwa na umri wa takribani miaka 78 .
Tarehe hiyo ya kuachiwa inazingatia muda ambao tayari ametumikia pamoja na uwezekano wa kupunguziwa kifungo kutokana na nidhamu njema gerezani. Ingawa bado inaweza kubadilika iwapo kutakuwa na rufaa au marekebisho ya kisheria.
Akiwa na miaka 59 sasa Kelly amekuwa akihangaika kisheria kujinasua katika gereza hilo. Agosti 2025 aliwasilisha ombi akiitaka Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali ya Marekani iondolewe kwenye kesi yake.
Ombi hilo lilikataliwa na Jaji Martha Pacold, aliyelitaja jaribio hilo kuwa “la kupitiliza” na kusema halina msingi wowote wa kisheria.
Maombi mengine ambayo yalikataliwa na jaji huyo ni kuomba kupewa kifungo cha nyumbani. Hatua hiyo imepelekea kukosa pakutokea huku hukumu yake ikibaki palepale.
Akiwa gerezani, Kelly ameendelea kujihusisha na muziki ambapo siku chache zilizopita kipande cha sauti yake kilisambaa mitandaoni akiimba wimbo wa Chris Brown ‘It Depends’. Aidha Brown na mtayarishaji Riley waliachia kipande hicho huku wakiandika ujumbe usemao…
“Bado ndiye Mfalme wa R&B bila mpinzani!!! Siwezi kusubiri kusikia muziki mpya kutoka kwake!!!” aliandika Riley.
Kwa sasa, Kelly anatumikia kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa mtandao (racketeering) na unyanyasaji wa kingono kwa watoto kesi ambayo alihukumiwa mwaka 2023.