Kibaha. Shule ya Sekondari Msangani Two iliyopo Manispaa ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, imeweka mkakati wa kupanda miche zaidi ya 20,000 kila mwaka ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha na kuhifadhi mazingira ya shule na jamii inayozunguka eneo hilo.
Mkakati huo umeelezwa kupitia risala ya shule iliyosomwa na mwanafunzi wa Kidato cha Tatu, Janeth Victor, wakati wa tukio la upandaji wa miti 2,000 lililofanyika leo Jumanne Januari 27, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa risala hiyo, shule tayari imeanza utekelezaji wa mkakati huo kwa kununua viriba 32 vya miche ya miti ya matunda na kivuli, hatua inayolenga kuboresha uoto wa asili, mazingira ya kujifunzia pamoja na kuchangia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Matukio mbalimbali ya upandaji miti Shule ya Sekondari Msangani. Picha na Sanjito Msafiri
Uongozi wa shule umeomba kuungwa mkono na serikali pamoja na wadau wa mazingira ili kufanikisha azma hiyo, huku ukipendekeza kuanzishwa kwa ushindani wa upandaji miti kati ya shule na shule ili kuongeza hamasa ya utunzaji wa mazingira na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za asili.
Akizungumza katika tukio hilo, Kamanda (TFS) Kanda ya Mashariki, SACC Mathew Ntilicha, amesema pamoja na upandaji huo, wa miti TFS inaendelea kufanya ufuatiliaji wa kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa na kudumu, akisisitiza kuwa ushiriki wa jamii ni muhimu katika kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
“Tumewwka mikakati mbalimbali ikiwemo kugawa miti bure kwa jamii na Taasisi mbalimbali ili ipandwe na kutunzwa lengo ni kuboresha mazingira”amesema
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ni taasisi ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii yenye jukumu la kusimamia, kuendeleza na kulinda rasilimali za misitu na nyuki nchini, ambapo mchango wake unajumuisha uhifadhi wa mazingira, udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi, ulinzi wa vyanzo vya maji na kukuza uchumi wa wananchi kupitia rasilimali za misitu.
Akihitimisha tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, amesema wilaya inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwemo kuvutia wawekezaji wanaozalisha nishati safi kama gesi, pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa taasisi zinazojihusisha na masuala ya uhifadhi wa mazingira.
“Maeneo mengi ya nchi kumekuwa kukisikika taarifa za uharibifu wa mazingira na misitu lakini sisi kwa uoande wetu tunataka kusikia taarifa kuhusu uboreshaji wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti na hili linawezekana na tumeshaanza”amesema
Simon amesema juhudi hizo zinalenga kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanaendana na utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.