
Harakati ya Ansarullah ya Yemen, leo imetoa indhari kwa kukumbusha shambulio lake la huko ililofanya kwa mafanikio dhidi ya meli ya mafuta ya Uingereza ya “Marlin Luanda” katika Ghuba ya Aden kufuatia ukiukaji wa mzingiro wa majini uliowekwa na harakati hiyo dhidi ya Israel,
na kuionya Marekani na washirika wake kuhusu utayari kamili wa Sanaa na uwezo wa hali ya juu wa majini ilionao wa kukabiliana na manowari ya nchi hiyo ya kubebea ndege za kivita ya “Abraham Lincoln” katika maji ya eneo hilo.
Afisa mmoja wa jeshi la Yemen mjini San’aa ametangaza kwamba, “Harakati ya Ansarullah ya Yemeni haitaruhusu meli yoyote ya Marekani wala manowari zake za kubebea ndege za kivita zikaribie Bahari Nyekundu na Bahari ya Arabia na inavichukulia vyombo hivyo kuwa ni tishio kwa Yemen.”
Msimamo huo umetangazwa sambamba na kushtadi mivutano ya kijeshi ya kikanda na kuwasili kwa manowari ya kubebea ndege za kivita ya Marekani ya “Abraham Lincoln” katika eneo hili.
Kwa mujibu wa gazeti la Lebanon la Al-Akhbar, afisa huyo wa jeshi amesisitiza kuwa “Vikosi vya Ulinzi vya Yemeni vimeongeza kiwango cha utayari wao na utayarifu wa kivita hadi kiwango cha juu zaidi kufuatia hatua za hivi karibuni za Marekani, hususan tangazo lake la kupeleka “kundi la manowari za mashambulizi” zinazoongozwa na manowari ya kubebea ndege za kivita ya “Abraham Lincoln”, ambayo huko nyuma ilikuwa shabaha na mlengwa wa mashambulizi ya Yemen.”
Kuhusiana na hilo, Brigedia Jenerali Aziz Rashid, mtaalamu wa masuala ya kijeshi aliye karibu na harakati ya Ansarullah amesema, “Vikosi vya Wanamaji vya Yemen vinafuatilia kwa karibu harakati za adui katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Arabia na vitachukua hatua kuzima jaribio lolote la kuweka kwenye eneo hilo kundi la manowari za mashambulizi linaloongozwa na manowari ya Abraham Lincoln.”
Jenerali Rashid amekumbusha kuwa, manowari hiyo ya kubebea ndege iliwahi kulengwa katika vipindi vya huko nyuma ilipokuwepo katika eneo hilo, ikiwa ni sehemu ya operesheni ya Marekani dhidi ya Sana’a na katika jibu ililotoa Yemen la kuitetea na kuiunga mkono Palestina.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa kijeshi, utayari wa sasa wa Yemen ni mkubwa zaidi kulinganisha na vipindi vilivyopita, na endapo Marekani na utawala wa Kizayuni zitashadidisha mgogoro huo watakutana na “mshtukizo mkubwa wa kijeshi” unaowasubiri…/