Dar es Salaam. Sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Coastal Union juzi imeifanya KMC kuendeleza rekodi yake isiyovutia ya kuwa timu ambayo haijapata ushindi kwa muda mrefu zaidi katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Matokeo hayo yameifanya KMC ifikishe siku 135 bila kupata ushindi kwenye Ligi, tangu ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Dodoma Jiji FC, Septemba 17, 2025.

Baada ya ushindi huo pekee ambao hadi sasa KMC imeupata kwenye ligi, timu hiyo imecheza mechi 10 mfululizo bila kushinda ambapo imetoka sare mara mbili na kupoteza michezo nane.

Baadhi ya wachezaji wa Singida Black Stars, wakijiweka sawa katika Uwanja wa mazoezi. Picha na Singida BS

Katika chati ya timu ambazo hazijapata ushindi kwa muda mrefu kwenye Ligi Kuu, Singida Black Stars inashika nafasi ya pili nyuma ya KMC ambapo yenyewe ina siku 122 ilizopitisha bila kupata pointi tatu katika mechi moja.

Tangu Singida Black Stars ilipoifunga Mashujaa FC kwa bao 1-0, Septemba 30, 2025, timu hiyo katika mechi tano zilizofuata imetoka sare kwenye mechi tatu na kutoka sare mbili.

Mshambuliaji wa KMC, Rashid Chambo akijaribu kumtoka beki wa Coastal Union, Andrew William katika mechi ya Ligi Kuu iliyomalizika kwa sare ya 1-1. Picha na KMC

Mbeya City ni timu nyingine ambayo haijapata ushindi kwa muda mrefu kwenye Ligi Kuu msimu huu ambapo haijaonja ushindi kwa siku 104 huku timu ya Tanzania Prisons ikiwa haijapata ushindi kwa siku 101.

Kocha wa KMC, Mohammed Abdallah ‘Baresi’ alisema kuwa ana imani timu yake itaanza kupata matokeo mazuri hivi karibuni.

“Timu inaimarika na wachezaji wanaonyesha utayari wa kupambania ushindi hivyo Mungu akisaidia tunamaini mambo yatakuwa mazuri,” alisema Baresi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *