Kusainiwa Mkataba wa Maelewano wa Islamabad na Marais wa Iran na Marekani kunashiria mwisho wa mojawapo ya mivutano na makabiliano makubwa zaidi kati ya nchi hizi mbili.

Kusainiwa mkataba huu wa maelewano na Marais Donald Trump wa Marekani na Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunaashiria mwanzo wa awamu mpya katika milingano ya kijiopolitiki katika eneo la Asia Magharibi na katika mfumo wa kimataifa. Awamu ambayo labda inadhihirisha zaidi kuliko huko nyuma kwamba uwezo haufafanuliwi tu katika mtazamo wa ukubwa wa maghala ya silaha, bali pia katika uwezo wa mapambano, uthabiti wa kitaifa, na kugeuzwa vitisho kuwa fursa. Mkataba wa Maelewano ya Islamabad umetiwa saini katika hali ambayo Marekani na utawala wa Kizayuni, baada ya siku arubaini za vita vya kulazimishwa dhidi ya Iran, hazikuweza kufikia malengo yao ya msingi wala ya daraja la pili.

Malengo ya wazi ya vita hivi yalikuwa ni kubadilisha uwiano wa ndani ya Iran, kudhoofisha nguvu ya taifa, kuibuliwa mpasuko kati ya dola na wananchi, na hatimaye kuilazimisha Tehran ikubali masharti ya adui ikiwa katika nafasi dhaifu. Lakini kilichotokea uwanjani kilitoa picha tofauti kabisa. Muqawama wa kijamii, mshikamano wa kitaifa, na nguvu ya uzuiaji ya Iran viliwageuzia kibao maadui.

Jamii ambayo ilidhaniwa kuwa ilikuwa imepoteza uimara wake chini ya mashinikizo ya miongo kadhaa ya vikwazo vya kulemaza na gharama za vita, ilithibitisha wazi katika medani ya mapambano kwamba tishio la nje linaweza kuwa sababu nzuri ya kuimarisha mshikamano wa ndani.

Ukweli huu ulikuwa ujumbe muhimu zaidi wa kimkakati wa vita kwa eneo na ulimwengu mzima kuwa si rahisi kuifuta Iran katika ramani ya nguvu kubwa duniani. Miaka 47 ya mashinikizo ya juu, kutengwa, vitisho vya kijeshi, vikwazo vya kiuchumi, vita vitatu vya kulazimishwa na njama za kuidhibiti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sasa imekabiliwa na ukweli mchungu kwa maadui kwamba Iran ni mchezaji muhimu na imara wa kikanda, ukweli halisi wa kijiopolitiki, sehemu isiyoweza kutenganishwa na milinganyo ya usalama ya Asia Magharibi na ulimwengu. Kwa mtazamo huu, Mkataba wa Maelewano ya Islamabad sio makubaliano ya kumaliza vita tu; bali ni hati inayopaswa kuchukuliwa kuwa “ya kukubalika hali halisi mpya ya nguvu.”

Kukubalika ukweli kwamba usalama wa kieneo hauwezekani bila Iran, uthabiti katika Ghuba ya Uajemi haupatikani bila ushiriki wa Iran, uhuru wa usafiri wa baharini katika Lango-Bahari la Hormuz haupatikani bila kuzingatiwa nafasi ya Tehran, na wala hakuna mradi wowote wa usalama unaolenga kuitenga Iran utadumu. Mkataba huu unaweza kuchukuliwa kuwa hatua ya kuanzia ya kufafanua upya uhusiano wa Iran na Marekani baada ya miaka 47 ya uhasama. Bila shaka, utakuwa ujinga mkubwa kudhani kwamba kwa kutiwa saini hati hii, kutoaminiana kihistoria ambako kumekuwepo kati ya pande hizi mbili kumekwisha. Kumbukumbu ya pamoja ya Wairani imejaa uzoefu wa mapinduzi ya 1953, vikwazo vya kulemaza, kujiondoa Marekani katika mikataba ya awali, na vitisho vya kijeshi vinavyoendelea. Kwa sababu hii, hakikisho kuu la kutekelezwa mkataba huu sio matumaini ya kisiasa, bali ni kanuni ya “ahadi mkabala wa ahadi” na uwezo wa Iran wa kulipiza kisasi.

Katika ngazi ya kikanda pia, matukio haya yamebeba ujumbe muhimu. Nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, ambazo katika miaka ya nyuma zilitumai kupata utulivu, ustawi na maendeleo ya kiuchumi chini ya mwavuli wa usalama wa Marekani, sasa zimetambua zaidi kuliko wakati mwingine wowote udharura wa kuunda mifumo ya usalama ya kieneo kwa ushiriki wa Iran. Uzoefu wa vita vya karibuni umeonyesha kuwa uwepo wa vikosi vya kigeni sio tu haudhamini usalama, bali pia unaweza kuwa chanzo cha matatizo ya kiusalama. Kwa hivyo, wazo la usalama wa pamoja wa kikanda linaweza kuhamishwa kutoka pembezoni mwa masuala muhimu hadi katika kitovu cha muktadha wa siasa za Asia Magharibi.

Kimataifa, Mkataba wa Maelewano ya Islamabad unaonyesha mabadiliko ya taratibu katika mpangilio wa kimataifa. Ulimwengu ambao sasa mataifa makubwa yanakabiliwa na vizingiti vikubwa vya kimkakati kuliko miaka ya nyuma, na ambapo matumizi ya njia za kijeshi si mdhamini wa moja kwa moja wa kufikiwa malengo ya kisiasa. Matukio haya yanaweza pia kuchukuliwa kama ishara ya mabadiliko kutoka siasa za “mashinikizo ya juu” hadi “kudhibiti ushindani na kukubali hali halisi ya mambo.” Njia iliyo mbele bila shaka haitakuwa rahisi. Mazungumzo juu ya kuondolewa vikwazo, masuala ya nyuklia, mifumo ya utekelezaji, na dhamana ya utekelezaji bila shaka utakuwa mtihani mgumu. Lakini umuhimu wa kihistoria wa mkataba huu wa maelewano unaonekana katika ukweli kwamba baada ya miongo kadhaa ya vitisho na makabiliano, na kupitia vita vyenye gharama kubwa na mapambano ya kitaifa, hatimaye ramani ya njia imebuniwa kwa ajili ya kuimarisha mafanikio ya Iran na kumaliza mzunguko wa uhasama. Islamabad, kwa maana hii, sio tu jina la jiji ambalo linahusishwa na mkataba wa maelewano yaliyopo. Ni nembo ya wakati wa kihistoria ambapo mantiki ya ufutaji upande wa pili iliondolewa na mahala pake kuchukuliwa na mantiki ya kukubali ukweli wa mambo. Ukweli wa amambo ambao taifa la Iran, lililazimisha milingano ya kieneo na kimataifa kuukubali, kupitia mapambano na ukakamavu wake. Iran haiwezi kupuuzwa, haiwezi kufutwa, na wala mustakabali wa kanda hauwezi kupangwa bila kuzingatia nafasi yake muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *