Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo, Mathew amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha wananchi wa Mji wa Ngudu wanapata huduma ya maji safi na salama kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa wilayani Kwimba.

Akijibu swali la Mbunge wa Kwimba, Mheshimiwa Cosmas Mtesigwa Bulala, aliyeuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kuanza ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji safi katika Mji wa Ngudu, Mhandisi Kundo amesema Serikali kwa sasa inaendelea na mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika eneo hilo.

Ameeleza kuwa mradi huo unahusisha ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kutoka Muhalo–Mwamashimba hadi Runele lenye urefu wa kilometa 25.4, ambapo utekelezaji wake umefikia wastani wa asilimia 15.

Mhandisi Kundo amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama katika jumla ya maeneo 14, yakiwemo maeneo ya Mji wa Ngudu, hivyo kupunguza changamoto ya uhaba wa maji kwa wananchi.

Aidha, amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha maandalizi ya Mradi wa Usambazaji wa Maji ndani ya Mji wa Ngudu, ambao utahusisha ulazaji wa mabomba yenye jumla ya urefu wa kilometa 17.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, mradi huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 32,000 wanaoishi katika mitaa 11 ya Mji wa Ngudu, ikiwemo Ngumo A, Ngumo B, Nguduruguru, Stand Mpya, Chamera, Bugakama, Iramba A, Iramba B, Ichefu, Majengo Mapya na Budula.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *