Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer ametoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran.

Akizungumzia chokochoko za Rais wa Marekani, Donald Trump katika eneo la Asia Magharibi, hasa kupeleka kundi la meli za kivita katika Bahari ya Arabia na tishio la kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, Starmer, amekariri madai ya kisiasa kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran, akisema kwamba “kipaumbele nambari moja” ni kuizuia Tehran kupata silaha ya nyuklia.

Keir Starmer, ambaye alikuwa safarini nchini China, alidai Alkhamisi, Januari 29 kwamba: “Changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba Iran haipati mpango wa nyuklia, na sote tunakubaliana kabisa kuhusu hilo na tunafanya kazi na washirika ili kutimiza lengo hilo, hilo ndilo lengo kuu la kile ninachofanya na washirika wetu.”

Alipoulizwa kama hatua za kichochezi za Marekani ni sahihi, Waziri Mkuu wa Uingereza amedai: “Sote tunakubaliana kwamba kuhakikisha Iran haipati mpango wa nyuklia ndio kipaumbele nambari moja, na hicho ndicho tunachofanyia kazi.”

Keir Starmer

Ni muhimu yya kukumbusha kwamba mradi wa kuzalisha nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani wa Iran umekuwa chini ya mashinikizo ya kisiasa na tuhuma zisizo na msingi za Magharibi kwa miaka mingi. Kabla ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, nchi za Magharibi zilijaribu kulihusisha suala hilo la masuala ya usalama na kuchukua hatua kadhaa dhidi ya Iran kwa kutumia vikwazo na vitisho vya kijeshi. Hata hivyo kufungwa faili la uwezekano wa mpango wa nyuklia wa Iran kuwa na malengo ya kijeshi  hapo mwaka wa 2015 kuliondoa kisingizio hicho.

Baada ya kusaini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran ilitekeleza majukumu yake yote, lakini Marekani ilijiondoa kwenye makubaliano hayo Mei 2018, na licha ya ahadi nyingi, Ulaya pia hatimaye haitekeleza wajibu na majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Matokeo yake, Iran ilichukua hatua za kupunguza uwajibikaji wake ndani ya mfumo wa kutetea haki zake ndani ya mkataba wa JCPOA. Mazungumzo ya kufufua JCPOA mwaka wa 2021 pia yalifeli kutokana na sera za ukwamishaji za nchi za Magharibi.

Katika wakati huu muhimu sana, ushirikiano wa Keir Starmer na Donald Trump katika kutoa madai mapya dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran unaonekana na waangalizi wengi kama ishara ya ushirikiano kati ya London na Washington katika vita vipana vya kisaikolojia na propaganda chafu. Ushirikiano huo si muhimu tu katika mtazamo wa kisiasa, lakini pia unaonyesha kwamba serikali ya Uingereza imefadhilisha kuingia ndani ya mfumo wa sera ya Marekani ya mashinikizo na propaganda za hali ya juu katika kipindi hiki cha sasa, badala ya kufuata sera huru na za kjitegemea. Uchunguzi wa sababu za ushirikiano huu unatoa picha ya wazi zaidi ya malengo yaliyo nyuma ya misimamo huu.

Sababu ya kwanza ni jaribio la Starmer la kuimarisha nafasi yake katika uwanja wa sera za kigeni. Akihitaji kuonyesha msimamo imara na ushirikiano na washirika wa jadi wa Uingereza, Keir Starmer anajaribu kujionyesha kama mchezaji hai kwa kuchukua misimamo mikali dhidi ya Iran na mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani. Mbinu hii inaonekana kama njia ya kuimarisha nafasi ya Uingereza katika masuala ya kimataifa, hasa wakati huu ambapo uhusiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantiki una umuhimu mkubwa kwa London. Starmer pia anajaribu kupata mazingatio maalumu kutoka kwa Trump kupitia misimamo hiyo.

Sababu ya pili inahusiana na hali ya ushindani wa kisiasa wa ndani wa Uingereza. Starmer anafanya jitihada za kuhakikisha kwamba hatuhumiwi na mrengo wa kihafidhina au vyombo vyake vya habari kuwa ni mpole na laini mbele ya Iran. Kuchukua msimamo mkali dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran ni aina ya ngao ya kisiasa ya kupunguza mashinikizo ya ndani na kujilinda kutokana na ukosoaji.  

Keir Starmer

Jambo la tatu ni jitihada za kujaribu kuwa na ushawishi katika mazingira ya kimataifa yanayoizunguka Iran. Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani na Uingereza zimejaribu kuanzisha propaganda chafu za vyombo vya habari ili kuudhihirisha mpango wa nyuklia wa Iran kama tishio na kutayarisha njia ya mashinikizo makubwa ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya Tehran. Kukariri madai yasiyo na msingi kuhusu shughuli za kuzalisha nishati ya nyuklia za Iran ni sehemu ya vita hivyo vya kisaikolojia, ambavyo vinalenga kuibua shaka katika maoni ya umma duniani na kudhoofisha msimamo wa Iran katika mazungumzo yanayowezekana kufanyika katika siku zijazo.

Sababu ya nne ni jitihada za kupindua maoni ya umma kutoka kwenye migogoro ya ndani ya Uingereza. Serikali ya Starmer inakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi, uhamiaji na masuala ya kijamii; na kuchukua misimamo mikali katika sera za kigeni ni njia ya kuvutia umakini wa vyombo vya habari na kupindisha mwelekeo wa vyombo hivyo kutoka kwenye matatizo ya ndani na kuyahamishia kwenye masuala ya kimataifa. Kutoa madai mapya dhidi ya Iran katika mazingira kama hayo kunaweza kupiga ndege wawili kwa jiwe moja: kutunisha msuli na kupotosha na kupindisha mwelekeo na mazingatio ya vyombo vya habari.

Kwa ujumla, msimamo wa Starmer na Trump kuhusu suala la mpango wa nyuklia wa amani wa Iran unaonyesha kwamba sera ya mashinikizo dhidi ya Tehran inasalia kuwa mhimili thabiti katika mkakati wa Magharibi. Ushirikiano huo umeundwa kwa msingi wa mahesabu ya kisiasa, propaganda chafu na na masuala ya kijiopolitiki badala ya uhalisia wa kiufundi na kisheria wa mpango wa nyuklia wa Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *