
Moshi. Abiria waliokuwa wakisafiri kati ya Rombo na Moshi pamoja na maeneo mengine ya Mkoa wa Kilimanjaro wamekwama kwa zaidi ya saa tatu baada ya vurugu kuzuka katika eneo la Uuwo Mwika, Wilaya ya Moshi.
Vurugu hizo zilianza takribani saa 10 jioni leo, Juni 12, 2026, zikihusishwa na kifo cha dereva wa bodaboda aliyedaiwa kugongwa wakati wa purukushani zilizotokana na gari linalodaiwa kuwa la polisi kutoka Rombo kumkimbiza.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa dereva huyo alihisiwa kubeba dawa za kulevya aina ya mirungi, ingawa madai hayo bado hayajathibitishwa rasmi na vyombo vya usalama.
Baada ya tukio hilo, wananchi na madereva wa bodaboda kutoka maeneo ya mpakani mwa Wilaya za Moshi na Rombo walikusanyika na kufunga barabara kuu ya Rombo–Moshi, hatua iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri waliokuwa wakiingia na kutoka katika wilaya hizo mbili.
Polisi waliofika eneo la tukio walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu waliokuwa wamekusanyika na kuzuia barabara, kabla ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, kufika eneo hilo akiwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa ajili ya kurejesha utulivu.
“Nipo eneo la tukio, siwezi kuzungumza kwa sasa, nitazungumza baadaye,” amesema Mnzava alipoulizwa kuhusu tukio hilo.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema barabara imefunguliwa na shughuli za usafiri zinaendelea kama kawaida.
“Ni kweli barabara ilifungwa kutokana na fujo zilizokuwepo, lakini kwa sasa imefunguliwa na shughuli zinaendelea. Hatujajua mzizi wa jambo hilo kwa sababu uchunguzi bado unaendelea,” amesema Maigwa.
Kamanda huyo amesema jeshi hilo litasubiri matokeo ya uchunguzi ili kubaini uhalisia wa tukio na hatua zinazostahili kuchukuliwa.
“Nasi tumesikia kama inavyosikika kuhusu sababu za tukio, lakini tutafanya uchunguzi kubaini uhalisia, na hiyo itaweka ukweli wote hadharani. Tukibaini kuna jambo lolote limetendwa kinyume na sheria, tutafuata njia ya haki bila kujali nani amehusika,” amesema.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa eneo hilo, kufungwa kwa barabara kulisababisha msongamano mkubwa wa magari ya abiria na mizigo kwa muda wa zaidi ya saa tatu kabla ya hali kurejea kuwa tulivu.
Endelea kufuatilia Mwananchi…