
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na Afrika Kusini uliingia katika mgogoro mkubwa na usio wa kawaida jana Ijumaa, baada ya pande zote mbili kutangaza maafisa wa kidiplomasia wa kila upande kuwa watu wasiofaa na kuwaamuru waondoke ndani ya saa 72.
Hatua hii inatambuliwa kuwa kilele cha mvutano unaoendelea kati ya pande hizo mbili, hasa baada ya vita vya Israel na mauaji ya kimbari ya utawala huo dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, na vilevile hatua ya Afrika Kusini ya kuifungulia Israel mashtaka katika mahakkama za kimataifa kwa mauaji ya Wapalestina.
Kuongezeka huku kwa nvutano wa kidiplomasia kunakuja katika muktadha wa mfululizo wa ukiukwaji wa kanuni za kidiplomasia ambao Afrika Kusini imeutaja kama changamoto ya moja kwa moja kwa mamlaka yake ya kujitawala.
Serikali ya Afrika Kusini ilitangaza jana Ijumaa kwamba Ariel Seidman, kaimu mkuu wa ubalozi wa Israel mjini Pretoria, ni “mtu asiyetakika” nchini humo na imemtaka aondoke ndani ya saa 72.
Wizara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini imesema katika taarifa rasmi kwamba uamuzi huo umechukuliwa “baada ya mfululizo wa ukiukwaji wa usiokubalika wa kanuni na kaida za kidiplomasia,” jambo ambalo imelitaja kuwa ni changamoto ya moja kwa moja kwa mamlaka ya kitaifa ya Afrika Kusini.
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kwamba ukiukwaji huu wa sheria unajumuisha utumiaji wa mara kwa mara wa majukwaa rasmi ya mitandao ya kijamii ya Israel kufanya mashambulizi ya matusi dhidi ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Pia imemtuhumu mwanadiplomasia huyo wa Israel kwa kujihusisha na mienendo inayodhoofisha itifaki za kidiplomasia na hali ya kuaminiana kwa pande mbili.
Ariel Seidman ameshikilia wadhifa wake tangu balozi wa Israel alipoondolewa Afrika Kusini mnamo Novemba 2023, baada ya Pretoria kuwaondoa wanadiplomasia wake huko Tel Aviv kufuatia kushamiri vita na mauuaji ya kimbari huko Gaza mnamo Oktoba 2023.
Israel pia kwa upande wake imemtangaza mwakilishi mkuu wa kidiplomasia wa Afrika Kusini huko Tel Aviv, Shaun Edward Byneveldt, kuwa mtu asiyestahili na kumwamuru aondoke ndani ya saa 72.
Mgororo wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili uzishadidi baada ya Afrika Kusini kuwasilisha mashtaka dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki huko The Hague, tarehe 29 Desemba 2023, ikiituhumu kufanya mauaji ya kimbari huko Palestina.