Leo ni Jumamosi 27 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1447 Hijria mwafaka na 13 Juni 2026.

Miaka 756 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 27 Dhul-Hijjah mwaka 691 Hijria, aliaga dunia Sheikh Muslihuddin Saadi Shirazi, malenga mtajika wa mtaalamu wa mashairi na nathari za lugha ya Kifarsi.

Baada ya kuhitimu masomo ya utangulizi ya elimu za fasihi na dini katika mji alikozaliwa wa Shiraz, Saadi alisafiri kuelekea Baghdad akiwa bado kijana. Katika madrasa ya Nidhamiyah ya mji huo alijifunza elimu maarufu za zama hizo; na baada ya kuhitimu alisafiri kuelekea ardhi za Sham, Palestina, Hijaz, Roma na nchi zingine.

Wakati wa safari zake hizo, Saadi alipata kujuana na watu wa jamii tofauti; na kutokana na aliyoyasikia na aliyojionea, alitumia ustadi wake wa ushairi kusanifu mashairi ya kuvutia. Hatimaye alirudi alikozaliwa huko Shiraz alikoendelea kusanifu na kuanza kualifu vitabu kwa kutumia uzoefu na tajiriba ya miaka 30 ya kusafiri na kutalii miji na nchi mbalimbali pamoja na kujuana na watu wa aina tofauti.

Mnamo mwaka 655 Saadi alihitimisha uandishi wa kitabu chake adhimu cha masuala ya tabia na malezi cha Bustan, ambacho mashairi yake aliyatunga akiwa safarini. Ndani ya kitabu hicho, anazungumzia masuala ya haki na uadilifu, kufanya ihsani, unyenyekevu, upendo, kukinai, malezi, toba n.k. Athari nyingine maarufu ya malenga huyo mtajika wa Iran ni Golestan.

Mahali alikozikwa Saadi katika mji wa Shiraz, kila siku hupokea wapenzi na maashiki wa lugha na fasihi ya Kifarsi kutoka kila pembe ya dunia.   *****

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita muwafaka na tarehe 13 Juni 1921 katika miaka ya mwanzo ya usimamizi wa Uingereza huko Palestina, ilianza harakati kubwa ya kwanza ya wananchi katika ardhi yote ya Palestina dhidi ya Wazayuni.

Harakati ya wananchi hao wa Palestina ilibainisha upinzani wao dhidi ya siasa za kikoloni za Uingereza pamoja na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Wazayuni waliokuwa wakiishi Palestina.

Katika fremu ya sera hizo za Uingereza mwaka 1923 kulikuwa na Wazayuni 35 elfu huko Palestina na kabla ya kuundwa utawala bandia wa Israel mwaka 1948 idadi hiyo ilikuwa zaidi ya laki sita.    ****

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita sawa na tarehe 13 Juni mwaka 1944, kombora la kwanza la ardhi kwa ardhi la Ujerumani ya Kinazi lililojulikana kwa jina la V-1 lilishambulia ardhi ya Uingereza, katika Vita vya Pili vya Dunia.

Kabla ya hapo Ujerumani ilikuwa ikiishambulia ardhi ya Uingereza kwa njia ya anga. Baada ya vita hivyo, nchi nyingine duniani zilitengeneza makombora ya aina hiyo kwa teknolojia ya kisasa zaidi.   ****

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, inayosadifiana na 23 Khordad 1359 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kufanya mabadiliko katika vyuo vikuu hapa nchini, alitoa amri ya kuasisiwa Baraza la Mapinduzi la Kiutamaduni.

Katika ujumbe wake, Imam Khomeini MA aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuratibu na kuandaa mipango na mitalaa katika kozi mbalimbali za vyuo vikuu inayokwenda sambamba na mafunzo ya utamaduni tajiri wa Kiislamu.   ******

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Khordad 1362 Hijria Shamsia, Bi. Nusrat Amin, faqihi na mfasiri mkubwa wa Qur’ani Tukufu alifariki dunia katika mji wa Esfahan ulioko katikati mwa Iran.

Bi. Nusrat Amin aliutumia muda wake wote katika kuishughulikia Qur’ani Tukufu na kufanikiwa kufasiri kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu katika juzuu 15 na kuandika vitabu vingine vingi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni Al Sayr Wassuluk, Njia ya Saada na Nafahaat Rahmaniyya.    ****

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *