
Iran inapinga vitisho na kushurutishwa na ina azma thabiti ya kufanya mazungumzo, kuheshimiana pande mbili na kutekelezwa diplomasia kwa manufaa ya pande zote. Haya yameelezwa na Rais Masoud Pezeshkian huku Washington ikiendelea kutoa vitisho vya kijeshi dhidi ya Tehran.
Rais Pezeshkian ameeleza haya jana Ijumaa alipowasiliana kwa simu na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki. Viongozi hao wawili wamejadili hali ya mvutano inayoongezeka katika eneo la Magharibi mwa Asia na kutahadharisha dhidi ya hatua za kichochezi na za kuibua moto wa vita.
Marais wa Iran na Uturuki wamebadilishana mawazo kuhusu matukio ya sasa ya kikanda na kusisitiza haja ya mawasiliano ya kidiplomasia na kufanyika mazungumzo ili kuyapatia ufumbuzi masuala mbalimbali.
Rais Masoud Pezeshkian amesema kuwa Iran imejikita katika mazungumzo, kuheshimiana, kupinga vitisho na matumizi ya nguvu, na kushikamana na mantiki ya manufaa kwa ajili ya pande zote.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki amemweleza Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, kwamba Ankara iko tayari kuchukua jukumu la kuziwezesha Iran na Marekani kupunguza mivutano.
Marais wa Iran na Uturuki wamewasliana kwa simu baada ya Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kufanya ziara mjini Istanbul Uturuki kwa ajili ya mazungumzo ya ngazi ya juu na maafisa wa Ankara kuhusu matukio ya kikanda na uhusiano wa pande mbili.