Mwaka mmoja tu uliopita, ripoti kuhusu Myanmar zilikuwa zimejaa dhana na tetesi kwamba Tatmadaw, neno la Kiburma linalomaanisha jeshi, huenda lilikuwa limefikia ukingoni.
Leo, miaka mitano tangu utawala wa kijeshi uipindue serikali iliyochaguliwa kidemokrasia Februari 1, 2021 na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyojaa umwagaji damu, mazungumzo hayo yamefifia karibu kabisa.
“Uvumi wa mapema mwaka 2024 kuhusu kuanguka kwa utawala sasa uko kabisa nyuma yetu,” alisema Anthony Davis, mchambuzi wa masuala ya ulinzi na usalama wa machapisho ya Janes.
Katika mwaka uliopita, jeshi limerejesha miji muhimu na njia za biashara kaskazini-mashariki ambazo zilikuwa zimechukuliwa na muungano wa makundi matatu yenye silaha. Pia limejenga upya vikosi vilivyokuwa vimepungua kutokana na vifo na wanajeshi kukimbia, na limefanyauchaguzi wa awamu mbalimbali, uliokamilika Jumapili.
“Wako katika nafasi nzuri zaidi tangu mapinduzi ya kijeshi,” alisema Kyaw Htet Aung, mkuu wa utafiti wa migogoro, amani na usalama katika Taasisi ya Mkakati na Sera–Myanmar (ISP-Myanmar).
Wachambuzi wanahusisha sehemu kubwa ya kurejea kwa nguvu kwa utawala wa kijeshi na China.
China na Urusi zaingilia kati
Kabla na baada ya mapinduzi, Beijing ilijenga mahusiano na Tatmadaw pamoja na makundi ya wachache wa kikabila yenye silaha yanayotawala maeneo magumu ya mpakani na China, ikisaidia kuyapa silaha pande zote.
Hata hivyo, baada ya mashambulizi makubwa ya makundi matatu hayo mwishoni mwa 2023 na mapema 2024 yaliyolishinda jeshi kaskazini-mashariki, Beijing ilibadilisha msimamo wake kwa kasi na kuunga mkono utawala.
Baada ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, katika mji mkuu Naypyitaw Aprili 2024, Beijing iliyalazimisha makundi ya kikabila yenye silaha kusitisha kuunga mkono wanamgambo waliotokea baada ya mapinduzi, ilizuia biashara ya mpakani kwa waliokaidi matakwa yake, na kulazimisha makundi mawili kuingia kwenye usitishaji vita na kuondoka kwa sehemu katika maeneo waliyodhibiti.
“China imegeukia kwa nguvu sana kuunga mkono utawala huu wa kijeshi hasa kwa sababu waliogopa ungeweza kweli kuanguka,” alisema Matthew Arnold, mtafiti mgeni katika Shule ya Uchumi ya London (LSE). “Kiwango cha msaada wa China kwa junta kimekuwa kikubwa sana.”
Davis aliongeza kuwa Urusi pia imekuwa muhimu katika kulifanya jeshi kuwa na ufanisi zaidi vitani kwa kusaidia kuboresha mbinu za mapigano na kufanya matawi yake mengi yashirikiane vyema.
“Kuna washauri wa Urusi Naypyitaw na pia uwanjani. Pia kuna Kamati ya Pamoja ya Kupambana na Ugaidi kati ya Myanmar na Urusi, inayoongozwa na watu wakubwa kutoka pande zote mbili, na iliyo na jukumu muhimu la uratibu,” alisema.
Jeshi la Myanmar pia limeagiza teknolojia ya droni kutoka China na Urusi, hatua iliyoruhusu Tatmadaw kufuta, kama si kubadili kabisa, faida ambayo makundi ya waasi yalikuwa nayo awali katika matumizi ya droni.
Watawala wa kijeshi wa Myanmar pia wameanzisha kampeni kali ya kuandikisha wanajeshi tangu katikati ya 2024, jambo lililoimarisha idadi ya wanajeshi ambayo ilikuwa imepungua. Davis anasema kampeni hiyo imeongeza takribani wanajeshi wapya 90,000, ingawa wengi wao hawajapata mafunzo ya kutosha na hawana motisha.
Hakuna dalili ya mwisho wa mapigano
Hata hivyo, hakuna kati ya hayo kinachoonekana kuipeleka Myanmar karibu na mwisho wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo tayari vimesababisha, kwa baadhi ya makadirio, vifo vya takribani watu 92,000 na kuwafanya zaidi ya milioni 3.3 kuyahama makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Takwimu za migogoro zinazofuatiliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kijeshi ya London zinaonyesha kupungua kwa taratibu kwa vurugu tangu kilele chake mwishoni mwa 2023. Hata hivyo, bado zilirekodi zaidi ya mapigano, milipuko au mashambulizi 800 katika mwezi wa Desemba pekee.
Shirika la Armed Conflict Location and Event Data (ACLED) lenye makao yake Marekani pia lilihesabu rekodi ya visa 40 vya “ukatili” uliofanywa na jeshi mwaka 2025 — mashambulizi dhidi ya raia yaliyosababisha vifo vya watu 10 au zaidi.
Tatmadaw bado inadhibiti chini ya nusu ya nchi na ililazimika kufuta upigaji kura katika wilaya nyingi wakati wa uchaguzi wa mwaka huu. Chama cha Union Solidarity and Development Party kinachoungwa mkono na jeshi kilitangaza ushindi Jumapili, ingawa Umoja wa Mataifa na serikali kadhaa za Magharibi zimeutaja uchaguzi huo kuwa wa kinafiki.
Upinzani unaendelea kushikilia
Licha ya uchaguzi na mafanikio ya utawala wa kijeshi, mapigano yanaendelea katika maeneo mengi, yakiwemo maeneo ya kati ya Myanmar yanayokaliwa zaidi na kabila la Bamar. Vikosi vya upinzani bado vimegawanyika, lakini vinaonyesha dalili za uratibu bora zaidi.
Mwezi uliopita, vikosi 19 vya People’s Defense Forces (PDFs) viliunda muungano unaoitwa Spring Revolution Alliance, vikidai kuwa na hadi wapiganaji 15,000 na kutafuta ushirikiano na makundi makubwa zaidi ya kikabila yenye silaha.
Mapema mwezi huu, PDFs kadhaa zilianzisha kile ambacho Davis alikiita wimbi “lisilo la kawaida” la mashambulizi ya pamoja dhidi ya kambi za kijeshi huko Bago. Ingawa jeshi liliwatimua, alisema operesheni hiyo ilionyesha maendeleo muhimu katika uratibu kati ya makundi ya waasi.
“Mgawanyiko wa vita tofauti bado haujaisha, lakini kuna ufahamu kwamba uratibu unahitaji kuharakishwa,” alisema Davis.
Jeshi lilikuwa na matumaini kwamba uchaguzi ungepunguza vurugu. Arnold, hata hivyo, ana shaka, akisema amekuwa “ameshangazwa” kwamba makundi yenye silaha hayajaanza kujisalimisha kwa junta kwa pamoja au hata kwa sehemu baada ya miaka mitano ya umwagaji damu, hata kama ni kwa ahadi za malipo ya kifedha.
“Hakuna kati ya hayo kinachotokea Myanmar, na kwangu hilo linaonyesha bado kuna dhamira kubwa ya kuliondoa jeshi madarakani kabisa,” alisema.
Baadhi ya makundi, Arnold aliongeza, yameingia katika makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano na utawala wa kijeshi.
Mwaka ujao utakuwa wa maamuzi
Miaka mitano baada ya mapinduzi, wachambuzi wanakubaliana kuwa hakuna upande unaoonekana kuwa karibu kushinda au kushindwa vitani hivi karibuni, wala kurudi nyuma kutoka kwenye mapambano.
“Hawaoni njia mbadala nyingine, kama mazungumzo,” alisema Kyaw Htet Aung wa ISP-Myanmar. “Bado wanafikiri wanaweza kupata udhibiti kupitia ushindi wa kijeshi.”
Katika mwaka ujao, alisema atakuwa akiangalia jinsi mapigano yatakavyoendelea katikati ya nchi, ambako jeshi bado inadhibiti maeneo mengi. Arnold wa LSE alisema atakuwa akiangalia China na kiwango ambacho itakuwa tayari kwenda mbali zaidi kuiunga mkono serikali isiyopendwa sana.
Davis wa ACLED alisema kuwa tangu ziara ya Wang Yi mwaka 2024, Tatmadaw “imeshughulikia masuala ya idadi na ubora kwa umakini mkubwa.”
Aliongeza kuwa hatima ya vita vya wenyewe kwa wenyewe huenda ikategemea zaidi uwezo wa makundi ya upinzani kuimarisha uratibu wao na kuanza kutumia droni za “first-person-view” zinazotumia nyaya za fiber-optic, ambazo zimebadilisha vita nchini Ukraine.
“Hivyo basi, Tatmadaw haitapoteza vita hivi,” alisema. “Swali ni, je, wanaweza kuvishinda? Jibu litategemea kile ambacho upinzani utaweza kufanikisha katika mwaka ujao.”
