
Polisi jijini Kinshasa, hivi leo walitumia mabomu ya machozi, risasi za moto na mpira kuwatawanya mamia ya wafuasi wa upinzani waliokuwa wakijaribu kuandamana kuelekea nje ya bunge la kitaifa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Maandamano haya yalikuwa yameitishwa na vuguvugu la upinzani la C64 linalopinga marekebisho ya katiba ambayo wanasema yanalenga kumfanya rais Felix Tschisekedi aendelee kusalia madarakani.
Hata hivyo, polisi walikuwa wamepiga marufuku maandamano hayo waliyosema ni batili na tangu asubuhi mamia ya askari wenye silaha walikuwa wametumwa kuzunguka barabara kuu zinazoelekea kwenye ukumbi wa bunge.
Hata hivyo kufikia majira ya mchana, mamia ya wafuasi wa upinzani wakiongozwa na aliyewahij kuwa mgombea urais nchini humo, Martin Fayulu, alijitokeza barabarani na kuanza kuelekea kwenye ukumbi wa bunge kabla ya kukabiliwa na nguvu ya polisi.
Upinzani ulipanga kupiga kambi nje ya ukumbi wa bunge la kitaifa, kama ishara ya kuendelea kupinga mchakato unaoendelea kwenye bunge la seneti, ambapo wabunge wanajadilij muswada wa masharti ya namna kura ya maoni itakavyofanyika, muswada huo ukiwa umeshapitishwa na bunge.
Akinukuliwa na jarida la Actualite.CD akiwa kwenye makao makuu ya chama chake alikozingirwa na polisi, Martin Fayulu amesema watu wawili wameripotiwa kuuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, akiwemo aliyekuwa katibu mkuu wa UDPS Jean-Marc Kabundi na Delly Sesanga rais wa chama cha ANVOL.