Amesema matokeo ya uamuzi huo yatakuwa pia na athari kwa wanasiasa wa Ulaya katika siku za usoni, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi akiushutumu umoja wa Ulaya kwa kuzidisha moto kwenye ukanda huo na kufanya kosa kubwa la kimkakati.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya walifikia maamuzi hayo jana Alhamisi kwenye mkutano uliofanyika mjini Brussels na mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Kaja Kallas alisema utawala wowote unaowaua maelfu ya watu wake unajiangamiza wenyewe.
Msimamo huo wa pamoja unaanzisha utaratibu wa kisheria wa kurasimisha tamko hilo linalochukuliwa kama ishara nzito kwa kuwa jeshi hilo tayari limewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kutokana na ukiukwaji wa haki za binaadamu
Iran yamuita balozi wa Ujerumani
Katika hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemuita Balozi wa Ujerumani nchini humo Axel Dittmann, na kulingana na mkurugenzi wa wizara hiyo, Jenerali Alireza Yousefi wito huo unafuatia matamshi ya Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz aliyoyataja kama uingiliaji usio na maana yoyote kwenye masuala ya ndani ya Iran.
Merz alipozungumzia hatua kali zilizochukuliwa na mamlaka dhidi ya waandamananaji katikati ya mwezi huu, alisema ikiwa mamlaka inaweza kusalia madarakani kwa kutumia nguvu, ni wazi imekwishaporomoka na kuongeza kuwa kilichokuwa kinashuhudiwa ni siku za mwisho za utawala wa Iran.
WHO: Watumishi na hospitali walishambuliwa wakati wa maandamano
Taarifa kutoka mjini Geneva zimesema shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO limearifu kwamba madaktari na hospitali nchini Iran walishambuliwa wakati wa maandamano yaliyogubikwa na vurugu kubwa Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Gebreyesus amesema hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za watumishi wa afya kushambuliwa na karibu madaktari watano wanashikiliwa, na kutoa wito waachiliwe mara moja.
Awali taarifa zilisema madaktari waliowasaidia waandamanaji waliojeruhiwa walikamatwa na baadhi ya majeruhi walidai kuchukuliwa hospitalini na vikosi vya usalama.
Huku hayo yakiarifiwa, mjini New York, Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Guterres ametoa wito wa diplomasia katika kusuluhisha wasiwasi unaoongezeka kati ya Iran na Marekani wakati vitisho vya uvamizi wa kijeshi vikitolewa na pande zote mbili, huku Rais Donald Trump akiishinikiza Tehran kufikia makubaliano ya nyuklia.
Guterres amewaambia waandishi wa habari kwamba kuna umuhimu wa kuwepo kwa mazungumzo yatakayozifikisha pande hizo kwenye makubaliano ya nyuklia na hilo ndilo litakalozuia mzozo unaoweza kuwa na athari mbaya sana kwenye ukanda huo. Mapema leo, Trump amenukuliwa akisema anapanga kuzungumza na Iran ili kupunguza mvutano uliopo.