Mawaziri wa ulinzi wa Japani na Korea Kusini wamekubaliana kuendelea na ushirikiano na ziara za pamoja kwa mazungumzo ya kila mwaka.
Waziri wa Ulinzi wa Japani Koizumi Shinjiro alikutana na mwenzake wa Korea Kusini, Ahn Gyu-back, kwa takribani dakika 50 Januari 30 katika Kambi ya Wanamaji ya Yokosuka ya Kikosi cha Kujihami cha Wanamaji cha Japani karibu na Tokyo.
Koizumi alisema mwanzoni mwa mkutano kwamba anataka iwe fursa ya kubadilishana maoni ya wazi na kuimarisha uhusiano wa kuaminiana.
Ahn alisema anatumai itasaidia kusonga mbele uhusiano wa pande mbili.
Mawaziri hao wawili walithibitisha kujitolea kwao kufanya kazi pamoja kwa ajili ya amani na utulivu katika eneo hilo, ambapo hali ya usalama imekuwa mbaya zaidi.
Walikubaliana kuendelea na juhudi kati ya nchi hizo mbili, na pia na Marekani, kuelekea kuondoa kabisa silaha za nyuklia kwenye Rasi ya Korea.
Pia walikubaliana kuhusu ziara na mikutano ya pamoja kila mwaka ili kukuza ushirikiano wa ulinzi na kubadilishana mawazo kati ya mataifa hayo mawili.