Mamlaka katika Ukanda wa Gaza zimesema watu zaidi ya 500 wamefariki katika mashambulizi ya Israel tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipoanza kutekelezwa mwezi Oktoba mwaka jana.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yalianza kutekelezwa mwaka jana kama awamu ya kwanza ya mpango wa amani.
Hata hivyo, Israel imekuwa ikifanya mashambulizi mara kwa mara, ikiishutumu Hamas kwa kukiuka makubaliano hayo. Siku ya Januari 31, jeshi la Israel lilisema limeshambulia kituo cha kuhifadhi silaha na maeneo mengine ya Hamas huko Gaza.
Vyombo vya habari vya Palestina vinasema watu 31 waliuawa katika maeneo ya kaskazini na kusini mwa ukanda huo wakati majengo na mahema yaliyokuwa yakiwahifadhi wakazi yaliposhambuliwa.
Mamlaka za afya huko Gaza zilisema siku ya Januari 31 kwamba idadi ya vifo tangu kuanza kutekelezwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano imefikia 509.
Hamas ilitoa taarifa ikiilaani Israel kwa “uhalifu wa kikatili” na “ukiukaji mkubwa” wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Mwezi uliopita Marekani ilitangaza kipindi cha mpito kueleka awamu ya pili ya mpango wa amani, ambao unalenga kuelekea kuondoa shughuli za kijeshi na kuanza ujenzi mpya.
Bodi ya Amani, chombo kinachoongozwa na Rais wa Marekani Donald Trump, ilizinduliwa ili kusimamia utawala wa mpito wa Gaza.
Lakini idadi ya vifo inaongezeka kutokana na mashambulizi ya Israel yanayoendelea.