
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameonya kwamba, vita vyovyote vitakavyoanzishwa na Marekani dhidi ya Iran vitageuka na kuwa vita vya kikanda.
Akihutubia mkutano na mkusanyiko mkubwa wa watu katika Husseiniya ya Imam Khomeini mjini Tehran, mkesha wa kuamkia miaka maadhimisho ya kumbukumbu ya 47 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kumbukizi ya kurejea nchini Iran Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini, Ayatullah Khamenei amezungumzia vitisho vya hivi karibuni vya Marekani na kusema: Matamshi ya hivi karibuni ya Marekani kuhusu vita na zana za kijeshi hayana mapya.
Imam Khamenei amesisitiza kwamba, vitisho na maonyesho ya nguvu za kijeshi kamwe hayatalitisha taifa la Iran. Ameeleza bayana kuwa, “Wakati mwingine wanazungumzia vita na ndege na meli za kivita; hili si jambo jipya,” akikumbuka kwamba maafisa wa Marekani walikuwa wameitishia Iran mara kwa mara hapo awali kwa kudai kwamba “machaguo yote yako mezani, ikiwa ni pamoja na chaguo la vita.”
Akirejelea vitisho vya Rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya Iran, Ayatullah Khamenei amesema, “Taifa la Iran halipaswi kuogopa mambo haya; watu wa Iran hawaathiriwi na vitisho hivyo.” Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia sababu mbili kuu za mzozo wa miaka 47 kati ya Iran na Marekani, ambazo anasema ni azma ya Washington ya kuitawala Iran na upinzani wa taifa la Iran kwa azma hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba, Iran haitakuwa mwanzilishi wa vita vyovyote, lakini ameonya kuhusu majibu thabiti kwa uchokozi wa maadui. Amesema, “Sisi sio wale tunaoanzisha [vita], na hatutaki kushambulia nchi yoyote, lakini taifa la Iran litatoa pigo zito kwa yeyote atakayelishambulia na kulinyanyasa.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu ameashiria ghasia za hivi karibuni hapa nchini Iran na kuyaeleza kuwa “sawa na mapinduzi,” akisema njama hiyo ililenga kuharibu vituo nyeti na muhimu vya kuendesha nchi.
Amesema washambuliaji walilenga vituo vya polisi, taasisi za serikali, suhula za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), benki, na misikiti, na hata kuchoma Quran Tukufu, akibainisha kuwa machafuko hayo hatimaye yalizimwa.
Ayatullah Khamanei amebainisha kuwa, Iran ina mali nyingi zenye thamani, ikiwa ni pamoja na mafuta, gesi, migodi mikubwa, na eneo lake la kimkakati, na kwamba utajiri na umuhimu huo huvutia macho ya uchu ya madola yenye tamaa, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yanataka kuitawala nchi hii.